KIUNGO wa Yanga, Khalid Aucho amefunguka akikiri kuwa mziki wa Azam ndio unaowanyima raha kwa namna wanavyokutana na upinzani mkubwa, huku nyota wa zamani wa Jangwani anayekipiga Azam FC, Feisal Salum akianika silaha zake hadharani akikisitiza kiu ya kuzinasa Simba na Yanga katika Ligi Kuu.
Fei ameendelea kuboresha rekodi katika ligi tangu akiwa na Azam, ikiwamo kuongoza kwa sasa katika wachezaji wenye kuhusika na mabao mengi akifunga manne na kuasisti tisa, akiifikia rekodi ya asisti msimu uliopita iliyowekwa na Kipre Junior aliyekuwa akiichezea Azam kabla ya kutimkia MC Alger ya Algeria.
Msimu uliopita wakati Kipre akiongoza asisti, Fei alishika nafasi ya tatu nyuma ya Stephane Aziz KI wa Yanga aliyeasisti nane na kuongoza mabao akitupia 21 kumzidi Fei (19) na asisti saba.
Akizungumza baada ya kuasisti mara mbili wakati Azam ikiifumua JKT Tanzania mabao 3-1, Fei Toto alisema moto wake unachangiwa na namna kikosi kinachocheza chini ya kocha Rachid Taoussi na mikakati waliyonayo kuhakikisha wanazikamata Simba na Yanga zinazochuana kileleni katika ligi.
Kiungo huyo alisema kipaumbele chake ni kutengeneza nafasi za mabao jinsi walivyofundishwa mazoezini na pia wanavyocheza, ndio maana hana mabao mengi kulinganisha na msimu uliopita, lakini amevuka asisti za msimu uliopita. Fei alisema kocha anaona yeye ndiye anaweza kufanya jukumu hilo na sio kwamba hatafunga ila ikitokea nafasi atafanya hivyo.
“Kocha amenipa kazi ya kutengeneza nafasi kwa wenzangu ili timu ipate ushindi mkubwa. Ila uwezo wangu wa kufunga unajulikana, nikiweza kufanya hivyo katika mechi zijazo rekodi zitajieleza. Kwa kuwa mabao niliyoyafunga msimu uliopita yanatosha kuelezea juu ya ubora wangu wa kufunga,” alisema.
Kuhusu Simba na Yanga, Fei alisema mipango waliyonayo ni kupambana zaidi kuzishusha timu hizo zinazofuatana nafasi ya kwanza na ya pili, huku Azam ikiwa ya tatu juu ya Singida Big Stars iliyokuwa uwanjani jana.
“Timu yetu inaendelea kupunguza makosa kama ambavyo tulivyo anza msimu kwa utulivu na tunakwenda sambamba na kuzikimbiza timu zilizo juu yetu kwenye msimamo na tutazipata tu,” alisema Fei, huku kocha wa Taoussi akimzungumzia mchezaji huyo na kusema ni mwenye kipaji kikubwa na anaweza kucheza nafasi nyingi ila anapendelea kumtumia kama namba 10.”
Kiungo wa Yanga, Aucho ameivulia kofia Azam akisema ni moja ya timu ambazo mara zote zimekuwa zikiwapa wakati mgumu katika michezo ambayo wamekuwa wakikutana nao.
Aucho aliyetumika Yanga kwa misimu mitatu anaonakana kuvutiwa na kiwango kinachojitokeza wakati Azam inakutana na Yanga, akisema mechi hizo huwa na ushindani mkubwa na mara nyingi zinachukua sura ya kipekee kama fainali ya Ligi ya Mabingwa.
“Mchezo wetu dhidi ya Azam huwa wa kiwango cha juu sana. Wanapokutana na sisi, hujitahidi sana na mara nyingi mechi hizo huwa ngumu. Kwa hiyo, kila tunapokutana na Azam tunajua ni mechi yenye changamoto kubwa, lakini pia inatufanya tuwe bora zaidi uwanjani,” alisema Aucho.
Azam ilikuwa timu ya kwanza kuifunga Yanga (1-0) msimu huu wa 2024/25 katika ligi ilipokuwa chini ya Miguel Gamondi.
“Ikiwa Azam wataonyesha juhudi kama hizo wanapocheza na timu nyingine, basi nadhani wanaweza kufika mbali. Kwa kuzingatia ubora na kasi wanayoonyesha wanapocheza dhidi ya timu kubwa, ni dhahiri wana uwezo wa kushindana katika mashindano makubwa kama Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanya vizuri zaidi,” alisema Aucho.
Misimu mitatu ya Aucho akiwa Yanga, amekutana na Azam mara 10 ikiwamo saba za Ligi Kuu, mbili za Ngao ya Jamii na fainali ya Kombe la Shirikisho, huku Yanga ikishinda mara nne, ikipoteza mbili na sare moja kwa Ligi ya Bara, pia ikishinda mara zote katika Ngao na Kombe la Shirikisho.