Josiah afichua siri ya Maguli

BAADA ya Geita Gold kuinasa saini ya mshambuliaji, Elias Maguli kutoka Biashara United, kocha wa timu hiyo, Amani Josiah amesema usajili wa nyota huyo ni wa kimkakati ili kuongezea makali safu yake ya ushambuliaji.

Nyota huyo amerejea ndani ya kikosi hicho alichokitumikia msimu wa 2023-24, huku akiandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la Ligi Kuu Bara, wakati Geita Gold ilipoifunga Singida Black Stars zamani Ihefu bao 1-0, Agosti 15, 2023.

Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah alisema uhamisho wa mchezaji huyo ni muhimu kwao kwa ajili ya kuongeza upana wa kikosi hicho sambamba na kuboresha safu ya ushambuliaji, ili kutimiza malengo ya kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu ujao.

“Ni moja ya mapendekezo yangu kwa benchi la ufundi na nashukuru wameweza kutimiza hilo, ukiangalia mwenendo wetu wa timu kiujumla sio mbaya, ingawa ni lazima tuboreshe maeneo yote muhimu kwa ajili ya kuendana na ushindani uliopo,” alisema.

Maguli aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo, Stand United, Simba, Ruvu Shooting, KMC, FC Platinum ya Zimbabwe, AS Kigali ya Rwanda na Dhofar Club ya Oman, tayari ameshafunga mabao matatu katika Ligi ya Championship kwa msimu huu.

Wengine waliojiunga na Geita ni aliyekuwa beki wa kulia wa Biashara United, Faustine Kulwa, kiungo wa zamani wa Yanga, Singida Black Stars zamani Ihefu na Mashujaa FC, Said Makapu na Ally Ramadhan ‘Kagawa’ aliyewahi kuichezea Kagera Sugar.

Related Posts