Kwa Katwila ni maeneo mawili tu

WAKATI klabu zikiendelea kuvuta silaha mpya kwa ajili ya kujiboresha, kocha wa Bigman, Zubery Katwila amesema hatokuwa na haraka katika kuwaingiza wachezaji wapya, licha ya kuhitaji kuboresha zaidi maeneo ya kiungo na mshambuliaji wa kati.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katwila alisema tayari ripoti yake ameshaiwasilisha kwa viongozi na wanaendelea kuifanyia kazi, huku akilenga maeneo hayo kutokana na upungufu uliopo kikosini humo ili kuendana na ushindani.

“Ukiangalia jedwali unaona kabisa udhaifu tuliokuwa nao, tumecheza michezo 13 lakini tumefunga mabao manane tu, sasa hii itoshe kuona wazi tuna changamoto kubwa ambayo tunahitaji kuifanyia kazi kwa haraka wakati tukienda mzunguko wa pili.”

Kocha huyo mzoefu aliyetamba na timu mbalimbali zikiwamo, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mtibwa Sugar, amejiunga na Bigman akichukua nafasi ya Fredy Felix ‘Minziro’, aliyejiunga na Pamba kuchukua mikoba ya Goran Kopunovic.

Timu hiyo zamani iliyofahamika kama Mwadui FC ya mkoani Shinyanga, katika michezo 13 iliyocheza imeshinda mitano, sare mitatu na kupoteza mitano, ikifunga mabao manane na kuruhusu mabao tisa, ikishika nafasi ya tisa kwenye msimamo kwa pointi 18.

Related Posts