KATIKA kuhakikisha TMA inafanya vizuri katika Ligi ya Championship msimu huu, kocha mkuu wa kikosi hicho, Maka Mwalwisi ameweka wazi kuridhishwa na safu yake ya ushambuliaji hadi sasa, huku akiwataka mabosi kutofanya usajili kwa mihemko.
Mwalwisi alisema hadi sasa safu ya ushambuliaji imeonyesha matumaini makubwa na licha ya changamoto za eneo la kujilinda, hawataingia sokoni ilimradi tu kusajili, kwa sababu ni ngumu katika dirisha hili dogo kupata wachezaji wenye ubora.
“Haina maana wachezaji wazuri hawapo ila ninachohofia ni kuleta wapya ambao watachukua muda mrefu kutengeneza balansi na wengine, tunaendelea kurekebisha taratibu eneo hilo hivyo, hata tusiposajili kwangu sina shaka na waliopo,” alisema.
Kocha huyo aliongeza, licha ya washambuliaji wa kikosi hicho kufanya vizuri wanapaswa kuongeza juhudi zaidi, kwani viungo wa timu hiyo wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga hivyo, ni jukumu lao kuzitumia ili kutengeneza motisha kwao.
Kikosi hicho kilichofunga mabao 22 katika michezo 14 iliyocheza, kinaongozwa na mshambuliaji, Abdulaziz Shahame mwenye mabao tisa sawa na Andrew Simchimba wa Geita Gold, wakizidiwa mawili na kinara, Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar aliyefunga mabao 11.