WAKATI kipa Diarra Djigui, Clatous Chama na Yao Kouassi wakiwekwa chini ya uangalizi maalumu wa kitabibu, nyota wawili wa Yanga, Maxi Nzengeli na Kennedy Musonda wamekoleza mzuka kwa kuanza kujifua mazoezini na wenzao wakitoka kuwa majeruhi na kukosa mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu.
Nyota hao wa kigeni sambamba na Aziz Andambwile walikuwa sehemu ya kikosi kilichokuwa kikijiandaa na mchezo wa leo dhidi ya Fountain Gate utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam baada ya kurejea kutoka kuwa majeruhi zaidi ya wiki mbili.
Akizungumza na Mwanaspoti juzi kwenye mazoezi ya timu hiyo iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Daktari wa timu hiyo, Moses Etutu alisema maendeleo ya wachezaji wote waliorejea mazoezini ni mazuri na wapo chini ya uangalizi wa kocha wa viungo ili kuwarejesha haraka kwenye ya ubora tayari kwa kuanza kutumika.
Dk Etutu alisema ili kuwaweka wachezaji hao wako katika hali nzuri na kutorudi katika shida ya kupata majeraha kwa uharaka watalazimika kuwapeleka kwa kocha wa utimamu wa mwili (fitness coach) ili kuwarudisha taratibu kabla hawajacheza mechi za mashindano.
“Tunafurahi kuona wachezaji watatu, Musonda, Maxi na Andambwile wamerejea mazoezini kwa uharaka tofauti na matarajio. Hii ni juhudi ya wachezaji wenyewe kujitunza na kujipa muda wa mapumziko, pia sisi kama madaktari tumefanya kazi yetu kwa usahihi,” alisema Dk Etutu.
“Kuhusiana na Diarra bado anaendelea kufanyiwa matibabu na ni mchezaji ambaye anahitaji muda zaidi ili kumrudisha katika ubora aliokuwa nao, huku Chama na Yao nao wakiwa pia chini ya uangalizi wangu wa kitabibu.”
Alisema hawana haraka na wachezaji hao kurudi uwanjani na kwa sasa wanapambana kuwaweka katika hali nzuri ili wakirudi wafanye kazi ya kuipambania timu.
Nyota hao wamekosa mechi tatu za Ligi Kuu Bara ikiwamo dhidi ya Mashujaa, Tanzania Prisons na Dodoma Jiji, huku wakitarajiwa pia kulikosa pambano la leo litakalopigwa saa 10:00 jioni.