Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Anna Mwakilima (24) mkazi wa Kijiji cha Mbuyuni Wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa miezi miwili, Juliana Kiwero.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akizungumza leo Jumapili Desemba 29, 2024 ofisini kwake, amesema tukio hilo lilitokea Desemba 22, 2024 na mtuhumiwa alitumia mbinu ya kuomba hifadhi kwa mama wa mtoto huyo, Aneth Mgaya (20).
Amedai kuwa, Desemba 21, 2024 mtuhumiwa alifika nyumbani kwa mama huyo na kumuomba hifadhi ya siku moja kwa madai, ametokea Mbeya Mjini na amefika kijijini hapo kwa shughuli za kibiashara na amekosa nyumba ya kulala.
“Desemba 22, 2024 saa 1.00 asubuhi mama wa mtoto, Aneth Mgaya aliamka alfajiri na kwenda kununua vitafunwa vya kunywea chai, akamwacha mtuhumiwa na mwanaye lakini baada ya kurejea hakuwakuta,” ameeleza kamanda huyo.
Amesema baada ya kufuatilia, jana Desemba 28, 2024 saa 12.00 jioni mtuhumiwa alikamatwa akiwa na mtoto huyo.
“Tulipomtia nguvuni na kufanya upekuzi, tumemkuta na kadi ya kliniki ya mtoto huyo aliyo mfungulia katika moja ya kituo cha afya (jina limehifadhiwa) na amebadilisha jina na kumuita Patricia Christopher Mkula. Ni jinsi gani mtuhumiwa alivyodhamiria kuiba mtoto ndani ya siku nane tayari alifanya taratibu za kumfungulia kadi ya mahudhurio ya kliniki na kumbadilisha majina,” amesema kamanda huyo.
Ametoa rai kwa wazazi na walezi kuchukua tahadhari kwa wageni wanaowapokea ili kuepuka vitendo vya wizi wa watoto na ukatili wa kijinsia dhidi yao.
“Polisi tutakuwa wakali kwa wazazi wazembe kwa sababu kumeibuka kasumba ya baadhi ya wazazi kutotekeleza wajibu wao wa malezi na makuzi ya watoto na kusababisha mmomonyoko wa maadili miongoni mwa jamii,” amesema kamanda huyo.
Mkazi wa Ilemi, Sikujua Stanley akizungumza na Mwananchi amesema ufike wakati sheria zitungwe za kuwawajibisha wazazi wanaozembea kutunza watoto wao.
“Sasa mtu kaja kwako humjui, unamkaribisha na mtoto unamuachia, ulimwengu wa sasa ni hatari sana kwa watoto,” amesema.