Mwanza. Serikali imemuokoa mtoto wa miaka miwili aliyedaiwa kufungiwa ndani na mama yake (18) kisha yeye kwenda virabuni kunywa pombe hadi asubuhi ya siku inayofuata.
Mama huyo anadaiwa kuwa na matatizo ya kisaikolojia kutokana na kuwa na mgogoro na mzazi mwenzake ambaye hata hivyo bado hajafahamika, yaliyomfanya kuwa mraibu wa pombe.
Akielezea kwenye mtandao wa X jinsi mtoto huyo alivyookolewa leo Jumapili Desemba 29, 2024, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema jana asubuhi alipokea ujumbe kutoka kwa raia mwema anayeishi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora akimwambia binti huyo amekuwa na tabia ya kumfungia ndani na kurudi siku nyingine.
Amesema ujumbe huo unaeleza kuwa, “kuna binti ana mtoto ila lengo lake ni kama anataka kumuua kwa sababu imekuwa ni tabia yake kumfungia ndani na kuondoka kwenda anakoenda na kurudi siku nyingine. Hivyo tunaomba msaada wenu tafadhali.”
Amesema baada ya kupokea ujumbe huo aliwasiliana na uongozi wa Mkoa wa Tabora, waliotuma maofisa wa dawati la jinsia kufuatilia.
“Ni kweli mama wa mtoto alikutwa na viashiria vyenye hatari kwa usalama wa mtoto ikiwamo malezi na makuzi kwa jumla, ana tabia ya kumfungia mtoto ndani na kwenda kunywa pombe hadi asubuhi.Mama mtoto huyo ana mgogoro na mzazi mwenzake,” amesema Gwajima.
Amesema mtoto huyo alichukuliwa na kukabidhiwa kwa ndugu huku polisi na maofisa wa ustawi wa jamii wakiendelea kumuhoji mama huyo.
Huku, akirejea tukio la mauaji ya mtoto Grayson Kanyenye (6) lililotokea Desemba 25, 2024 jijini Dodoma, baada ya mama yake kudaiwa kumuacha kwa bodaboda aliporudi alikuta ameuawa, Dk Gwajima amesema matukio ya usalama mdogo wa watoto yapo maeneo mengi nchini na ameitaka jamii kuyamulika.
“Natoa wito kwa wanawake na wanaume kuacha kufanya mambo yanayoweza kupelekea mimba ambazo haziko kwenye maandalizi ya utayari wa kufanya malezi na makuzi timilifu ikiwamo ulinzi wa mtoto na kupelekea usalama wao kuwa mdogo,”amesema.
Amesema mzazi au mlezi akishindwa kumlinda mtoto atawajibishwa kwa mujibu wa sheria, huku akizikumbusha kamati za ulinzi wa watoto kila wilaya na halmashauri kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji na kata kusimama imara kwenye nafasi zao kuelimisha na kuhamasisha jamii, kupokea taarifa na kuchukua hatua stahiki.
“Mwanajamii ukipata taarifa za usalama mdogo wa mtoto au watoto timiza wajibu wako wa kutoa taarifa Dawati la Jinsia na Watoto Polisi au kwa Ofisa Ustawi wa Jamii. Piga namba 116 saa 24 kila siku, Kituo cha Wizara 0766400168/ 0734986503/ 0262160250/ 0769608130 na WhatsApp 0744112233 siku na saa za kazi,
“Namba yangu kwa rufaa ya mwisho ni 0765345777. Namba za maofisa ustawi wa jamii mikoa yote zitatangazwa. Ukipiga ukaona haipokewi, andika ujumbe tuma baki na kumbukumbu,”amesema Dk Gwajima.
Akitoa maoni yake Mponda Ambrose amesema, “kama mama wa mtoto ana umri wa miaka 18 basi alipata mimba akiwa na umri wa miaka 17 kama hivyo ndivyo, basi aliyempa mimba awajibishwe ila hii haina maana alichokifanya ni sawa, sheria ichukue mkondo wake.”
Hata hivyo, Dk Gwajima amemjibu kuwa, “ili awajabishwe, lazima apatikane, na ili apatikane, lazima mama mtoto atutajie.”
Naye, Anold Kashaija amesema, “punguzeni masharti na rekebisheni sheria kwa wababa kuishi na watoto wao, kuna wanawake wanang’ang’ania watoto kisa wamewageuza vitega uchumi, wengine wanadai hawataki kulelewa na mama wa kambo, eti mnakiuliza kitoto under 14(chini ya miaka 14) kinataka kuishi na nani kati ya baba au mama.”
Akimjibu, Dk Gwajima amesema, “shida ni baba mwenyewe hajatuambia yuko wapi, hadi tuambiwe Iili naye tumsikilize.”