Mwaka 2024 unavyoacha huzuni katika sekta ya anga

Dodoma. Ajali ya ndege ya Jeju Air, Boeing 737-800 iliyotokea jana Korea Kusini na kusababisha vifo vya watu 179, huku wahudumu wawili wa ndege hiyo wakinusurika kifo, imefunga mwaka kwa kuwa ajali ya ndege iliyoua watu wengi zaidi mwaka 2024. Ajali nyingine za ndege zilizoua watu wengi ni iliyotokea Desemba 25, 2024, ambapo ndege ya Shirika la Ndege la Azerbaijan, Embraer 190AR, ilitunguliwa huko Aktau, Kazakhstan na kuua watu 38.

Pia, Agosti 9, 2024, ndege ya Voepass Linhas Aéreas ATR 72-500 ilianguka eneo la makazi, Vila Santa Fé nchini Brazili na kusababisha vifo vya watu wote 62 waliokuwemo ndani ya ndege.

Hadi kufikia ukingoni mwa mwaka 2024, takriban ajali 14 za ndege zimeripotiwa kutokea duniani na kusababisha jumla ya vifo vya watu 296, huku ajali nne kati ya hizo zikitokea barani Afrika.

Ajali ya ndege ya Jeju Air iliyotokea Desemba 29, 2024, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan, Korea Kusini, ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo mwaka huu.

Ajali hiyo ilitokea wakati ndege ya Jeju Air, ikiwa imebeba abiria 175 na wafanyakazi sita, ikitua kutoka Bangkok, Thailand.

Wahudumu wawili wa ndege hiyo, mwanamke na mwanaume, ndio pekee walionusurika kati ya watu 181 waliokuwemo ndani ya ndege. Ndege hiyo ilipata ajali baada ya kuacha njia yake kwenye uwanja huo wakati ikutua na kushindwa kusimama.

Kwa mujibu wa tovuti za ajali za ndege, zikiwemo 1001crash.com, mwaka huu umeandika rekodi ya ajali 14 za ndege duniani, ikiwemo ajali za Dakar, Senegal; Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC); Malakal, Sudan Kusini na Nairobi, Kenya.

Machi 5, 2024, ajali ilitokea Nairobi, Kenya, ikihusisha ndege za Safarilink Aviation Flight 53 (De Havilland Canada Dash 8) na Cessna 172.

Ndege ya Cessna 172 ilianguka na kusababisha vifo vya marubani wawili waliokuwemo, huku Dash 8 ikifanikiwa kutua salama.

Mei 9, 2024, Dakar, Senegal, ndege ya abiria aina ya Boeing 737 ilipata hitilafu ilipokuwa ikiongeza kasi ya kupaa kuelekea Bamako, Mali. Watu 11 walijeruhiwa, huku ndege hiyo ikiwa na abiria 79 na wahudumu sita.

Mei 5, 2024, Kinshasa, DRC, ndege ya mizigo aina ya Boeing 737-300 ilipata ajali baada ya tairi kupasuka wakati wa kutua. Hakukuwa na majeruhi, lakini ndege hiyo ilipata uharibifu mkubwa.

Mei 31, 2024, Malakal, Sudan Kusini, ndege aina ya Boeing 727-200 ikitokea Juba iligongana na MD-82 ilipokuwa ikitua. Mfanyakazi mmoja alijeruhiwa, huku ndege zote zikiharibika vibaya.

Miongoni mwa ajali za kushtua mwaka huu ni pamoja na ile ya Desemba 25, 2024, ambapo ndege ya Shirika la Ndege la Azerbaijan, Embraer 190AR, ilitunguliwa huko Aktau, Kazakhstan.

Watu 38 walikufa, huku 29 wakinusurika. Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Baku, Azerbaijan, kwenda Grozny, Urusi, lakini hali mbaya ya hewa iliwalazimu kutua dharura.

Novemba 25, 2024, Vilnius, Lithuania, ndege ya DHL Boeing 737-476SF ilipata ajali wakati wa kutua. Ndege hiyo iligonga ardhi, kuteleza mita 250, na kugongana na jengo la makazi. Moto uliozuka uliua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.

Agosti 9, 2024, Brazili, ndege ya Voepass Linhas Aéreas ATR 72-500 ilianguka katika eneo la makazi, Vila Santa Fé, ikisababisha vifo vya watu wote 62 waliokuwemo. Ndege hiyo ilitoka Cascavel kuelekea São Paulo.

Julai 12, 2024, Gazpromavia Sukhoi SSJ100-95 ilipoteza urefu dakika saba baada ya kuruka kutoka Lukhovitsy, Urusi, na kuanguka kwenye msitu. Wafanyakazi wote watatu walikufa.

Januari 2, 2024, huko Tokyo, Japan, ndege ya Shirika la Ndege la JAL Japan, Airbus A350-900, iligongana na ndege ya doria ya pwani wakati wa kutua. Watu watano kati ya sita waliokuwemo kwenye ndege ya doria walikufa, lakini abiria wote 379 wa ndege kubwa waliokolewa salama.

Latam Airlines Flight 800, Boeing 787-9, iliyokuwa safarini kutoka Sydney, Australia, kwenda Auckland, New Zealand, ilipata msukosuko mkubwa wa hewa, na abiria 50 walijeruhiwa. Licha ya tukio hilo, ndege hiyo ilitua salama Auckland.

Ripoti za awali zinaonyesha ajali nyingi za ndege mwaka 2024 zimetokana na hali mbaya ya hewa, hitilafu za kiufundi, na makosa ya kibinadamu.

Ajali hizi zimeathiri sekta ya usafiri wa anga kimataifa, zikiwemo kupoteza maisha ya watu na mali, na pia kuzua mjadala wa usalama wa ndege.

Katika Bara la Afrika, changamoto za miundombinu duni na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kudhibiti safari za anga zimeendelea kuchangia ajali.

Serikali nyingi zimeshauriwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya anga ili kuhakikisha usalama wa abiria na mali.

Related Posts