Netanyahu kufanyiwa upasuaji wa tezi dume leo

Israel. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kuondolewa tezi dume hii leo Jumapili. 
Upasuaji huo unafuatia kugunduliwa kuwa na ugonjwa huo, ofisi yake imetoa taarifa hiyo leo Desemba 29, 2024. 

Kwa mujibu wa mtandao wa Times of Israel Jumatano iliyopita, Netanyahu, mwenye umri wa miaka 75, alifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Hadassah huko Jerusalem, ambapo madaktari waligundua ugonjwa huo katika njia yake ya mkojo kutokana na kuongezeka kwa tezi dume.
Katika siku za nyuma ikiwemo Machi mwaka huu Netanyahu alifanyiwa upasuaji wa ngiri (hernia) na mwezi huo huo akaugua mafua ambapo alikosekana kazini baadhi ya siku.
Aidha mwaka jana, Netanyahu alifanyiwa upasuaji wa kuweka kifaa cha kusaidia mapigo ya moyo (pacemaker) na upasuaji huo ulifanyika wiki moja baada ya kulazwa hospitalini kwa kile alichosema wakati huo kuwa ni upungufu wa maji mwilini.

Mfululizo huo wa magonjwa ulisababisha uvumi miongoni mwa watu nchini humo wakihofu afya ya kiongozi huyo. 

Ingawa katika ripoti ya matibabu iliyotolewa Januari mwaka huu ilisema Netanyahu alikuwa katika hali ya kawaida kabisa ya afya, kwamba betri ya moyo aliyowekewa ilikuwa ikifanya kazi vizuri.

Katika upasuaji wa leo Netanyahu anatarajiwa kusalia hospitalini kwa siku kadhaa.

Wakati hayo yakiendelea kwa upande wa uwanja wa vita, jeshi la nchi hiyo limesema jana Jumamosi limekamilisha operesheni dhidi ya Hamas katika hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza na maeneo jirani.

Katika operesheni hiyo takriban washukiwa 240 liliowaita wa ugaidi walikamatwa, akiwemo mkurugenzi wa kituo cha matibabu na baadhi wanaoidaiwa kushiriki katika shambulio la Oktoba 7, 2023, kusini mwa Israeli.

Related Posts