Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imeanza kufanya mazungumzo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuja na mfumo wa kidijitali ili kuwafikishia vitambulisho Watanzania milioni 1.2 ambao hajavichukua.
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, tayari Nida imeanza kuvikusanya vitambulisho ambavyo havijachukuliwa kwa wilaya ya Temeke mkoa wa Dar es Salaam na kuandaa utaratibu wa kuhakikisha vinawafikia walengwa.
Nida imechukua hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa aliyoyatoa Desemba 17,2024 jijini hapa, akiipa taasisi hiyo miezi miwili kuhakikisha vitambulisho 1.2 milioni vinasambazwa na kuwafikia walengwa.
Mwananchi, ilipomuuliza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari kuhusu mazungumzo hayo katika majibu yake alidai Nida wanaweza kuzungumzia zaidi kwakuwa ni changamoto inayowahusu.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 29, 2024 Ofisa Habari wa Nida, Geofrey Tengeneza amesema wamechukua hatua hiyo ili kutekeleza maagizo ya waziri.
“Tumeanza kufanya mazungumzo na TCRA kuja na njia ya kuwafikia ambao hawajachukua vitambulisho vyao, watusaidie kujua namba wanazotumia kwa sasa changamoto iliyopo wengi namba walizoandika kila wakipigiwa hawapatikani,” amesema.
Tengeneza amesema walipofanya tathmini za awali walibaini wengi wakati wanajiandikisha hawakutumia namba zao walitumia za ndugu, huku akieleza katika mazungumzo yao na TCRA wanataka wawasaidie kujua namba zao za sasa wanazotumia.
“Tunajua moja ya mahitaji ya kupata laini ya simu lazima uwe na namba ya Nida, lakini wakati ule watu walikuwa wanatumia namba za ndugu kwakuwa waliokuwa wengi hawakuwa na simu,” amesema.
Tengeneza amesema wakishapata mawasiliano yao watatumia Tehama kwa kumtumia kila mmoja ujumbe mfupi wa kuwataka kwenda kuchukua vitambulisho vyao.
Tengeneza amesema kwa wale waliohama mathalani alijiandikisha eneo fulani kisha akahamia sehemu nyingine kuna utaratibu wa ndugu au jamaa kwenda kuwachukulia.
“Kama una ndugu au jamaa cha kufanya unaandika barua kwenda Ofisi ya Wilaya ya Nida ambako kitambulisho kipo kwa kumtambulisha uliyemtuma na amekuja kukuchukulia kitambulisho chako na huyo mtu anatakiwa kuandika barua na kuandika namba yake ya Nida,” amesema.
Amesema katika kupeleka barua lazima ziambatanishwe zote ya anayeenda kuchukua na anayemchukulia na akiwasilisha anapatiwa bila shida huku akiwasihi wenye muda wakavichukue.
Kuhusu vitambulisho kufutika maandishi, Tengeneza amesema tayari wameshatoa matangazo kwa wananchi wenye changamoto hiyo wavirejeshe katika ofisi za Nida kwenye wilaya iliyo karibu nao.
“Vikishakusanywa vitarejeshwa makao makuu kwa matengenezo kama wilaya iko mbali arejeshe ofisi ya serikali ya mtaa alipoenda kuchukua, kwa sababu watendaji wameshapewa maelekezo,” amesema.
Tengeneza amesema changamoto ya baadhi ya vitambulisho kukosa ubora ilijitokeza katika kipindi ambacho walikuwa wanazalisha kwa wingi na kuvigawa kwa umma.