ONGEA NA ANTI BETTI: Mchungaji anaamua nini kifanyike nyumbani kwangu

Sielewi kama huyu mke ni wangu au wa mchungaji. Naomba niweke sawa, ninaamini katika dini na sikosi kanisani kwa ajili ya ibada na maombi mengine. Pia sioni shida mke wangu kujikita katika masuala ya imani, changamoto ni namna mchungaji wa kanisa letu anavyogeuka kiongozi nyumbani kwangu, kwani mke wangu ndiyo mtu pekee anayemsikiliza kwa kila jambo.

Nilikuwa naona kuna changamoto hiyo, ila hivi sasa ni kama imezidi, kwani hivi karibuni tulipanga kununua eneo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nyingine, ajabu ni kwamba mke wangu alisema ngoja akamuulize mchungaji wetu kama hilo eneo linafaa kujengwa na sisi. Hilo pia siyo shida, majibu ya mchungaji yalibadili kila tulichokijadili kwa muda mrefu, alisema tusijenge eneo hilo na tusubiri wakati wa Mungu kujenga, mke wangu kalishikilia hilo anatamani fedha tulizokusanya kwa ajili hiyo akazitoe sadaka zote.

Sijajua nia ya Mchungaji ni nini kumueleza mke wangu hilo, pia nilipofikia sihitaji kujiuliza haya maswali kwani nimeshachoka.

Nilikuwa ninasikia tu wanawake wakiwaamini viongozi wa dini hawabadiliki ila huyu wangu amezidi, kila jambo lazima akamuulize kiongozi wa dini, amekuwa hakimu wa ndoa yetu. Huu mwaka wa nne tunalumbana tuongeze mtoto wa tatu hataki, kwa hili ninapata wasiwasi pengine kashauriwa na huyu kiongozi asubiri kwanza. Naomba ushauri nifanyeje?

Duh! Masuala ya imani ni magumu kidogo, kwani kila mmoja ana mtazamo wake na anajua anachokiamini na kinampa manufaa gani.
Ila bila kumung’unya maneno mkeo ana shida, hasa katika uelewa wake wa mambo na uwezo wa kufikiri.

Haiwezekani masuala ya familia, tena muhimu kama hilo akaulize kwa mchungaji.
Mchungaji pia amepata mtu wa kuchezea na hili linadhihirika kutokana na majibu anayompa, huwezi kumpangia jambo la kufanya mke wa mtu aliyekuja kukuuliza peke yake ilhali unajua ana mumewe waliyeamua pamoja.

Hivyo mkeo ana shida na mchungaji hana busara, kwani anajibu kama mpiga ramli, jambo ambalo kwenye imani limekatazwa.

Labda kama mtu mwingine tu angesema msijenge pale pana hili na lile kwa maana ya changamoto, labda eneo lina maji, mgogoro, halipitiki, mmebanana. Tofauti na hapo amekosea kutoa maamuzi kwa ajili ya familia ya wengine hata kama ameulizwa.

Kuwa makini sana, wachungaji wa aina hii wapo, wanaoacha kuhubiri neno la Mungu na kujiingiza kwenye mambo mengine.

Sitaki kusema moja kwa moja, ila ninachokiona huyu mchungaji hana nia nzuri na ndoa yako. Hakuna dhambi kuilinda, hivyo hakikisha unapunguza mazoea ya mkeo kumuona mchungaji wenu kama mtu wa mwisho kufanya maamuzi ya ndoa yenu.

Wanawake, kina mama, kina dada, mashangazi twendeni kwenye nyumba za ibada kuabudu na kujiweka karibu na Mungu badala ya kujiweka karibu na viongozi wa dini, tunawaweka mtegoni, ipo siku watajikuta wamesema maneno ya tamaa za kimwili kwa sababu tunawanyenyekea kwa namna tofauti kabisa. Tusiwachumishe dhambi hawa watu wa Mungu, tuheshimu ndoa na familia zetu.

Narudi kwako pia, ukiwa baba wa nyumba hakikisha kila kitu kinakuwa sawa, unaacha kujenga kwa sababu mkeo kakatazwa na mchungaji! Acha basi. Simama kiume usikubali mtu mwingine kutawala nyumba yako.

Related Posts