Radi yaua watano wa familia moja, yajeruhi sita Chunya

Mbeya. Watu watano kutoka jamii ya wafugaji wamepoteza maisha na wengine sita kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku.

Tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Isangawane, Kata ya Matwiga, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya na inaelezwa kuwa hili ni tukio la pili kwa mwezi huu ambapo radi iliyotokea awali  iliua mtu mmoja.

Diwani wa Kata ya Matwiga, Frank Mkondo akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Desemba 29, 2024 amesema tukio hilo lilitokea saa 6 usiku wa kuamkia leo ambapo watu hao walikuwa wamelala.

Amesema kitongoji lilipotokea tukio hilo, kimepimwa rasmi na Serikali ya Kijiji kwa ajili matumizi ya makazi.

“Mvua kubwa ilianza kunyesha saa 6:00 usiku na kudumu kwa takriban saa mbili, ikifuatana na radi kali, hali iliyosababisha vifo vya watu watano papo hapo na wengine sita kujeruhiwa, na watu hawa walikuwa wameweka kambi kwenye eneo hilo wakiwa na mifugo yao,” amesema.

Mkondo amesema alipokea taarifa kutoka kwa wananchi baada ya mvua kukatika, akielezwa kuhusu vifo hivyo na majeruhi waliokuwa wakihitaji msaada wa haraka. Viongozi wa kijiji walifika eneo la tukio na kushuhudia miili ya watu watano ikiwa chini, huku majeruhi wakipelekwa kupata huduma ya kwanza.

“Mpaka sasa, miili ya watu watano bado haijaondolewa eneo la tukio, lakini taratibu za uchimbaji wa makaburi zinaendelea,” ameongeza Mkondo.

Diwani Mkondo amesema majeruhi sita walipelekwa kwenye duka la dawa muhimu kijijini hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza.

Hata hivyo, Mwananchi ilihoji kwa nini majeruhi hao walipelekwa kwenye duka hilo badala ya zahanati au kituo cha afya, Diwani Mkondo amesema ni kutokana na eneo hilo kutokuwa na zahanati wala kituo cha afya.

Taarifa zinaeleza kuwa umbali kutoka kijijini hapo hadi kilipo kituo cha afya ni kilomita saba.

“Wananchi wengi wa kijiji cha Isangawane hutegemea maduka ya dawa muhimu kwa huduma za afya kutokana na umbali wa vituo vya afya na zahanati,” amesema.

Amesema pia changamoto ya miundombinu na jiografia ya Wilaya ya Chunya ilivyokaa, inakwamisha watu kuvifikika vituo vya afya na zahanati pindi wakipata dharura.

Mkondo ametoa wito kwa Serikali kusogeza huduma muhimu karibu na makazi ya wananchi, ikiwa ni pamoja na uwepo wa wataalamu wa afya wa kutosha.

Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga azungumzie hilo, amesema hana taarifa kuhusu tukio huku akiahidi kulifuatilia na atalitolea ufafanuzi.

                                                      

Akizungumza na Mwananchi Digital, mhudumu wa duka hilo muhimu la aliyeomba  hifadhi ya jina lake, amesema alipokea majeruhi watano waliopigwa na radi na kuwapatia huduma ya kwanza.

“Tulijitahidi kutoa huduma ya haraka na sasa wanaendelea vizuri, ingawa mmoja ameruhusiwa kurudi nyumbani tayari, wengine bado nawahudumia,” amesema.

Related Posts