Arusha. Wakati Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kikitoa tamko la kulaani kushambuliwa na kuuawa kwa Wakili Joseph Masanja, Wakili Peter Madeleka amesema ni wakati wa TLS kutumia sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata kujua chanzo cha kifo hicho na kukomesha vitendo hivyo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani alipotafutwa na Mwananchi leo Jumapili, Desemba 29, 2024, amesema uchunguzi umekamilika, lakini hawapo kwenye nafasi nzuri ya kueleza nini kipo kwa kuwa jalada litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi.
Taarifa ya TLS iliyotolewa jana, Desemba 28, 2024 na Baraza la uongozi la TLS na kusainiwa rais wa chama hicho, Boniface Mwabukusi imedai taarifa zilizowafikia ni kuwa Wakili Masanja aliokotwa eneo la Bwalo la Magereza, Manyara.
Imedai wakili huyo amefariki dunia Desemba 23, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi alikopelekwa kwa uchunguzi na matibabu zaidi na kuwa tukio hilo linaashiria ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, usalama wa mawakili na kuhatarisha misingi ya utawala bora wa sheria nchini.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Desemba 29, 2024, Wakili Madeleka amesema tukio hilo linapaswa kulaaniwa na watu wote wapenda haki na linapaswa kuchukuliwa hatua zaidi.
Ameshauri TLS ichukue hatua zaidi, ikiwamo ya kupeleka maombi maalumu kwa Mahakama ifanye uchunguzi kujua chanzo cha kifo hicho kwa kutumia sheria ya uchuguzi wa vifo vyenye utata.
“Mahakama ichunguze si Jeshi la Polisi, sisi TLS nadhani ni wakati wa kutumia sheria ile, ili kutoa uelewa kwa wananchi na kukomesha matukio kama haya. Mfano mimi niliitumia sheria hii kwenye kesi ya Stella Mosses aliyefia mahabusu akidaiwa kujinyonga,”
“Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni Kinondoni, ilitoa amri ya mwili huo kufukuliwa ili kufanyiwa uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake kilichotokea mwaka 2020 akiwa Kituo cha Polisi Mburahati,”amesema Madeleka.
Kwa upande wake, Kamanda Ahmed, amesema wao kama polisi wameshakamilisha upelelezi na wanasubiri hatua zaidi baada ya jalada kufikishwa kwa DPP.
“Sisi kama Polisi tumeshafanya uchunguzi wetu tumemaliza, ila kwa sasa hatuko katika nafasi ya kusema kuna nini. Kesho Jumatatu tunapeleka jadala kwa DPP na baada ya kupitiwa huko, maelekezo tutakayoyapata ndiyo tutajua tunasema nini,”amesema.
TLS imetoa wito kwa vyombo vya dola, hususani Jeshi la Polisi kuanzisha uchunguzi wa kina na haraka juu ya tukio hilo na kuhakikisha wahusika wanapatikana na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili kukomesha vitendo vya aina hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ilimtambua wakili huyo kuwa ni mwanachama wake mwenye namba ya uwakili 7664.
“Kwa mujibu wa majukumu ya TLS katika kuhakikisha ulinzi, haki na maslahi ya mawakili na usalama wao unazingatiwa wakati wote, tunalaani vikali shambulio hili lililosababisha mauaji ya wakili mwenzetu ambalo pia limeleta huzuni, hofu na woga miongoni mwa wanataaluma ya sheria na jamii kwa ujumla kuhusu usalama wa mawakili.
“Vilevile tunaitaka Serikali kuhakikisha inachukua hatua za dhati katika kuhakikisha usalama wa wanasheria na watetezi wa haki za biandamu, hakuna taifa linaloweza kufanikisha maendeleo endelevu,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa kwa kuzingatia mazingira ya mauaji hayo watashirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kufuatilia suala hilo na kuhakikisha upatikanaji wa haki na majibu sahihi ya tukio hilo.
“Tunatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wanataaluma wote kwa msiba huu mkubwa.Tunawaomba wote tuendelee kushikamana, kudai haki na kuhakikisha hatuyumbi katika misingi ya kutetea utawala wa sheria,” imeeleza taarifa hiyo.