Kijiji cha Makumbusho kimekuwa moja ya vivutio vya utalii wa ndani jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
Kijiji hicho chenye ukubwa wa ekari 15 kipo maeneo ya Makumbusho jijini humo kilianzishwa mwaka 1966, ikiwa ni wazo la Mwalimu Julius Nyerere.
Wazo la kuanzisha lilimjia baada ya watu wa kabila la Waha kujenga mfano wa nyumba zao za kimila katika uwanja wa maonyesho ya Sabasaba mwaka 1966.
Kwa usiyefahamu maonesho ya biashara hayo yalianza mwaka 1962 yakiwa na lengo la kukuza kilimo na ushirika na viwanja yalipokuwa maonyesho hayo yakifanyika viliitwa viwanja vya Wizara ya Biashara na Ushirika.
Hata hivyo, ilipofika mwaka 1978 Serikali iliunda Bodi ya Biashara ya Nje kupitia sheria yake namba 5 ya mwaka huo.
Bodi hiyo ilipewa mamlaka kushughulikia usafirishaji wa bidhaa za Kitanzania nje ya nchi na ilipewa pia dhamana ya kukuza ushirikiano wa biashara ya kimataifa kupitia maonesho ya kibiashara na kufanya utafiti kuhusiana na biashara.
Miaka ya hivi karibuni maonesho hayo yamekuwa yakishirikisha nchi zaidi ya 25 kutoka nje na kampuni zaidi ya 400, yakiwa sasa yanajulikana kwa jina la Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, huku viwanja vinavyotumika vikiitwa viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Nyerere.
Akisimulia sababu ya kuanzishwa kwake, Ofisa Elimu wa kijiji hicho, Wilhelmina Joseph, anasema ilikuwa mwaka mwaka 1966 ambapo kabila la Waha walibeba nyumba yao na kupeleka kwenye maonyesho hayo ya biashara.
Baada ya Mwalimu Nyerere kupita kwenye banda lao na kuiona nyumba hiyo, aliagiza kutafutwe eneo kwa ajili ya kuihifadhi nyumba hiyo, hivyo ikapelekwa katika eneo hilo na kuanzia hapo eneo likaitwa Kijiji cha Makumbusho na kilizinduliwa rasmi mwaka 1967.
“Kiutamaduni kabila hilo maisha yao ni ya kuhamahama, hivyo wanapokwenda eneo jingine huwa wanahama na nyumba yao, hivyo kuileta nyumba hiyo kwenye maonyesho kulimvutia hayati Nyerere,” anasema Wilhelmina.
Wilhelmina anasema kijiji hicho ni makumbusho ya wazi, kikiwa pia sehemu ya utalii, kutoa elimu kwa jamii kuhusu tamaduni mbalimbali zilizopo nchini na kuhifadhi urithi wa jamii ya Watanzania kwa kizazi kilichopo na kijacho kupitia ujenzi wa asili ya nyumba za makabila ya Tanzania.
Ofisa huyo anasema ndani ya kijiji hicho mbali ya kuwepo nyumba za asili 36 za makabila yapatayo 18, pia kuna vifaa vya asili vinavyopatikana ndani na nje ya nyumba zilizopo.
Pia katika kijiji hicho huwa kuna ngoma ya asili ambayo huchezwa kila siku eneo hilo.
“Aidha, ndani ya kijiji hicho kuna msitu mdogo wa ekari tano ambao umeuhifadhiwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiutamaduni.
“Shughuli hizo ni pamoja na ya mkole (yaani kumcheza mwali) ambapo jamii mbalimbali huenda kuwacheza wali wao katika msitu huo hasa kabila la Wamakonde ambao bado wanaendeleza tamaduni hizo,”anasema ofisa huyo.
Pia msitu huo anasema unahifadhiwa kwa ajili ya utoaji elimu kwa jamii, watu kuutumia kufanyia tafiti mbalimbali na kuwepo kwa mimea ya asili ambayo inatumika kwa dawa.
Wilhelmina anasema zipo changamoto mbalimbali zinazofifisha lengo la kuanzisha kijiji hicho, kubwa ikiwa ni ukosefu wa rasilimali fedha.
Pia mapokeo kwa jamii ambapo baadhi ya watu huamini kwenda kutembelea eneo hilo ni sawa na kupoteza muda.
‘’ Kinachoonekana ni ushamba bila kujua hiyo ni sehemu ya utamaduni wetu, ambapo ukifika hapo utasikia, utaona na utashika na kushiriki kwa namna moja au nyingine.
“Kama haitoshi, kubwa ni kwamba ukitembelea hapa ni sawa na umetembea Tanzania nzima kwa kuwa historia ya makabila yote zaidi ya 120 yanayopatikana Tanzania tunayo hapo,”anasema.
Hata hivyo pamoja na changamoto hizo, Wilhelmina anabainisha kuwa bado wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuandaa matamasha ya makabila mbalimbali.
“Ukiacha matamasha pia tunafanya programu mbalimbali wakiwamo wanafunzi, watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuwafundisha uchoraji, ufumaji, kucheza ngoma, michezo mengine ya asili kama kuruka kamba na kukimbia na magunia,’’ anaeleza.
Anaongeza: “Mchezo mwingine ni kucheza bao, mchezo unaochezwa na makabila mengi ambao lengo lake ilikuwa ni watu kukutana na kuwasiliana.
Gharama za kuingia kijijini hapo kwa Mtanzania mtu mzima ni Sh2500, mtoto Sh1,000.
‘’Endapo mtu atataka kutembezwa na kupewa maelezo na wahifadhi kumbukumbu, utapaswa kulipa Sh10,000.Wakati kikundi cha watu kuanzia 1-15 watalipia Sh15,000 na kwa wale watakaonzia 1-30 watalipa Sh20,000,’’ anasema.