Walalama mahindi yao kufyekwa, Serikali yajibu

Katavi. Wakati wakulima katika Kijiji cha Kagunga Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wakilia kufyekwa kwa mazao yao shambani, Serikali wilayani humo imefafanua tukio hilo, huku ikitoa tahadhari na maelekezo kwa wananchi.

Desemba 27 wakulima katika Kijiji hicho walijikuta katika taharuki kufuatia watu wasiojulikana kuvamia mashamba yao yenye ukubwa wa ekari 60 na kufyeka mahindi.

Akizungumzia tukio hilo leo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Onesmo Buswelu amesema mashamba hayo yamefyekwa baada ya kufanyika kwa doria katika vijiji vinane vinavyotekeleza mradi wa hewa ukaa, ambao umevamiwa na watu wanaoendesha shughuli za kilimo cha mahindi sambamba na bangi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Easter mpima-mkulima Kijiji cha Kagunga wilaya ya Tanganyika

“Ni kweli tumepata taarifa ya ekari zaidi ya 60 zilizokuwa zimelimwa mahindi ambayo yalikuwa yamefika hatua ya kuzaa zimefyekwa na tunafahamu msimu huu wa kilimo upo katikati ambapo kuna wakulima ambao wamekaribia kuivisha mazao yao na wengine wanaendelea na shughuli za kilimo,” amesema.

Akitolea mfano Kijiji cha Kagunga, Buswelu amesema walikutana mashamba ya mahindi yamelimwa kwenye eneo la uhifadhi yakiwa yamechanganywa na mimea ya bangi, jambo ambalo halikubaliki.

“Serikali ya Wilaya ilitenga maeneo ya wakulima, wafugaji na uhifadhi, hili la uhifadhi si la Serikali tu bali hata jamii inapaswa kushiriki kutunza misitu yetu na kuondokana na uharibifu wa mazingira,” amesema.

Amesema Wilaya ya Tanganyika inazungukwa na msitu wa Kamba unaokatiza katika vijiji vinane vinavyotekeleza mradi wa hewa ukaa.

“Naomba Watanzania wafahamu kuwa suala hili ambalo limetokea ni kutokana na doria ambayo iliendeshwa na vijiji vyote vinavyotekeleza mradi huu wa hewa ukaa, katika doria yao, walikutana na mashamba ya mahindi yamelimwa kwenye eneo la uhifadhi yakiwa yamechanganywa na dawa za kulevya aina ya bangi jambo ambalo halikubaliki kufanya kilimo cha bangi katika nchi yetu, ndiyo maana yamefyekwa,” amesema.

Hata hivyo, ametoa rai kwa wananchi na wanaofika Tanganyika kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, kufuata sheria huku akisisitiza hawawezi kuruhusu kilimo cha bangi na uharibifu wa mazingira bali kila mmoja anapaswa kuzingatia utaratibu na sheria za nchi.

Hili ni tukio la pili kutokea mkoani hapa, Februari mwaka huu katika Wilaya ya Mpanda zaidi ya ekari 10 za mahindi zilifyekwa kwa madai ya kutumika kuhifadhi wahalifu katika maeneo ya mjini.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumapili Desemba 29, 2024, baadhi ya wakulima hao wamesema wameshtushwa na tukio hilo wakieleza kuwa hawajui hatma ya maisha yao na familia kwa ujumla.

Ester Mpima amesema tangu wanaanza maandalizi ya kilimo hicho hawakupata usumbufu wowote, lakini wamesikitishwa hadi mazao yanafikia hatua ya kuchanua yanafyekwa.

“Tupo hapa miaka mingi tukiendelea na kilimo chetu na mradi wa hewa ukaa (kaboni) ulitukuta tukawa tunazingatia utunzaji mazingira na misitu, lakini tangu msimu umeanza hatukupata usumbufu hadi leo tunakutana na sintofahamu hii,” amelalamika Ester.

Amedai kupitia mradi huo waliambiwa watalipwa Sh700,000 kwa ekari moja tangu 2017, lakini mpaka sasa hawajalipwa chochote na wakifuatilia wanaambiwa wasubiri huku wakiendelea kulima.

Naye Christopher Kasemela amesema mradi huo wa hewa ya ukaa ulifika kijijini hapo 2017 na walielekezwa kuendelea na shughuli za kilimo wakati utaratibu wa fidia ukiendelea na hadi sasa hawajapewa kitu.

“Sisi hatukatai mradi tunachotaka ni stahiki zetu ikiwamo kututafutia maeneo mengine ya kwenda, tumetunza msitu huu na kama tungekuwa waharibifu, mradi huu usingekuwapo,” amesema Kasemela.

Naye Paul Moses amesema wamefuatilia kwa muda mrefu fidia lakini viongozi wanawajibu kuwa hakuna maeneo ya kuwapeleka.

Diwani wa Kata ya Kasekese, Paul Kakija amesema, awali wananchi  waliahidiwa kutafutiwa maeneo mengine yakiwamo ya makazi na kilimo ili kupisha eneo la mradi wa kaboni.

“Baada ya kukosekana maeneo ya kuwapeleka ilibidi waendelee na shughuli zao za kilimo, kitu ambacho hakitakiwi ni kuweka makazi.”

“Ninachoshauri katika hili ni kuzingatia makubaliano ya awali ili kila mmoja aishi kwa amani na utulivu, nitaendelea kufuatilia ili kila mmoja apate haki yake,” amesema diwani huyo.

Related Posts