Wimbi la udukuzi mtandao wa  WhatsApp

Dar/Moshi. Wimbi la udukuaji wa akaunti za WhatsApp limeanza kutikisa nchini huku watumiaji wa mtandao huo wakilalamika kutapeliwa baada ya kutoa ‘code number’ kwa wadukuaji hao.

Uchunguzi umebaini wengi walioingia katika mtego huo, walipigiwa simu na namba za simu kutoka Nigeria na wapigaji ambao huongea Kiingereza waliomba namba (code number) zilizotumwa na WhatsApp kwenye simu za waliodukuliwa.

Wataalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano ya Kompyuta (IT), waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wameeleza mbinu zinazotumiwa na wadukuaji na kuwataka watumiaji kuziepuka ili kuepuka kudukuliwa.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, wadukuaji hawawezi kukosekana duniani isipokuwa kinachotakiwa ni umakini wa mmiliki wa simu, kuhakikisha hatoi data zake kwa watu asiowafahamu.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabir Bakari ametoa tahadhari kwa Watanzania kuwa makini na kuchukua hatua stahiki katika ulimwengu wa kidijitali.

Dk Jabir amesema, mtu anapodukuliwa ni muhimu kutoa taarifa polisi.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama wa akaunti za kidigitali kwa kutumia nywila imara na huduma za uthibitisho wa hatua mbili (Two-Factor Authentication).

Pia, amewataka wananchi kuwa na umakini mkubwa kabla ya kubonyeza viungo visivyoeleweka au kutoa taarifa za siri mitandaoni.

Dk Jabir  amesema kinachofanyika siyo kudukuliwa bali wamiliki wa namba hutoa ushirikiano bila ya wao kujua.

“Ni yeye ametoa ushirikiano mtu akikupigia akakuambia kuna kikao cha kushiriki, kuna code (number) utatumiwa tutajie au anakupa link unafuata umeshirikiana nao,” amesema Dk Jabiri.

Amesema mara zote TCRA inasisitiza watu wafuate maelekezo yanayotolewa na mamlaka hiyo kila inapotoa elimu kwa wananchi kupitia programu mbalimbali mitandaoni na katika vyombo vya habari, ikiwamo redio na runinga.

“Unapokumbana na hali kama hii, hakikisha unatoa taarifa polisi ili pale namba yako itakapotumiwa vibaya, usije kuingia kwenye matatizo. Hii ni kwa sababu umempa mtu ruhusa ya kutumia namba yako, hivyo kila kitakachofanyika kinachukuliwa kama umetenda wewe mwenyewe,” amesisitiza Dk Jabir.

Hivi karibuni, kumeshuhudiwa ongezeko la malalamiko kutoka kwa watumiaji wa mtandao wa WhatsApp baada ya baadhi kudukuliwa akaunti zao na kutumiwa kusambaza viungo (links) vya kuwahamasisha watu kujiunga na makundi ya sarafu za mtandaoni.

Baadhi ya akaunti zilizoathiriwa zimetumika kusambaza picha zisizofaa, zikiwamo za ngono, kwenye makundi mbalimbali, hali inayoleta taharuki na kero kwa watumiaji wa mitandao.

Makundi ya kijamii kama ya wanazuoni, wachungaji, wanahabari, wanasheria na wananchi wa kawaida yamejikuta yakilengwa na wadukuzi kupitia ujumbe ‘code number’ mfupi kuingia kwenye akaunti zao.

Licha ya waathirika wengi kutoa taarifa kwa polisi au kuripoti moja kwa moja kwa WhatsApp, bado imeonekana kuchukua muda mrefu kupata ufumbuzi.

Athari za udanganyifu huu zimeendelea kuwa kubwa, hata baada ya akaunti husika kufungiwa.

Mwanazuoni mmoja aliyeingia kwenye mtego na kutuma  Sh500,000 kwa mtu aliyedhani ni mwenzake baada ya kupokea ujumbe wa dharura kupitia WhatsApp, amesema wadukuzi hawawezi kupata ufikiaji bila mtumiaji mwenyewe kutoa mwanya.

“Mtu anakutumia ujumbe WhatsApp kuwa amepata tatizo na asubuhi yake mliongea, ukiangalia kwenye profile yake ni picha yake ya siku zote. Unatuma pesa kumbe alishadukuliwa,” amesema mwanazuoni huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

“Ninashindwa kuelewa watu wa aina hii hawakamatwi. Kwa sababu hata kama laini ya simu iliyotumika kupokea fedha ni ya magumashi, si akamatwe wakala aliyeisajili,” amehoji.

Hata hivyo, Mwananchi ilipomtafuta Kamishna Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Kimtandao Makao Makuu Jeshi la Polisi, Joshua Mwangasa amesema uchunguzi wao umebaini kuwa wanaotekeleza vitendo hivyo ni Watanzania wanaojifanya wageni.

“Watu wanajifanya ni wageni lakini si kweli, anaiga ile lafudhi labda ya nchi kama Nigeria lakini wako ndani ya nchi, wanatumia Kiingereza katika kutekeleza azma zao ili kuonyesha umuhimu wa kile wanachokifanya, wakitumia Kiswahili inakuwa rahisi mtu kubaini,” amesema Mwangasa.

Amesema mbali na elimu inayotolewa ili kudhibiti suala hilo, pia wanafanya doria za mtandaoni kupitia majukwaa ya wazi kuangalia kama  kuna viashiria vya uhalifu wa mtandao.

“Pia, tuna mashirikiano ya kikanda na kimataifa ili kuhakikisha hata walio nchi jirani lakini wanafanya matukio yao Tanzania wanafikiwa, tunataka uchumi wa kidigitali ufanyike katika anga salama,” amesema.

Katika utendaji wa kazi zao wamekuwa wakishughulikia kesi mbalimbali huku akisema asilimia kubwa ya kesi ziko katika hatua ya upelelezi huku baadhi ya watu wakisaidiwa na Jeshi la Polisi kurejesha akaunti zao ili waweze kuendelea na mawasiliano.

Mwandishi wa habari mkongwe nchini, Joseph Kulangwa ambaye akaunti yake ya WhatsApp ilidukuliwa wiki mbii zilizopita, amesema siku aliyodukuliwa, alipigiwa simu na mtu akizungumza Kiingereza na lafudhi yake ikifanana na watu wa Taifa la Nigeria.

“Kuna mtu alinipigia simu anaongea Kiingereza cha Nigeria akaniambia kuna discussion (mjadala) unafanyika leo mtandaoni. Sasa sikutilia shaka kwa vile niko kwenye Chama cha Waandishi kutoka nchi za Afrika Mashariki,” amesimulia Kulangwa.

 “Kutokana na uwepo wangu huko, napokea simu kutoka kwa waandishi wa mataifa mbalimbali, nikajua pengine sikuwa aware (sikufahamu). Kwa hiyo akaniambia ananitumia code number na kweli nikaziona,” amesema.

“Huyo jamaa akaniambia hebu nisomee hizo namba, akaniuliza zina digiti sita? Nikazihesabu kweli akaniambia hebu nisomee nizihakiki. Ile namaliza kumsomea tu namba ya mwisho, akaunti yangu ya WhatsApp ikapotea.”

“Haikupita dakika tatu nikaanza kupigiwa simu ya kawaida, sasa naulizwa unatuma vitu gani kwenye makundi nikawaambia sio mimi, mimi sijatuma. Nikajua tayari. Nikawasiliana na WhatsApp wakasema nisubiri saa 11.”

Kwa mujibu wa Kulangwa, akaunti yake hiyo ilitumika kutuma viunganishi vya kujiunga na makundi kwa ajili ya sarafu mtandaoni na waliojaribu kuingia huko kwa kuamini yeye ndio ametuma na wanamwamini, baadhi walidukuliwa.

Mchungaji mmoja wa kanisa mashuhuri nchini, ambaye aliomba jina lake lisitajwe, ameeleza jinsi akaunti yake ilivyodukuliwa baada ya kupokea simu kutoka kwa mtu asiyemjua.

Amesema mtu huyo alidai kuna kikao cha mtandaoni na akamtaka mchungaji atumie namba maalumu za kuingia kwenye kikao hicho.

“Yule mtu alikuwa akiongea kwa Kiingereza na alionekana kushangaa, akaniuliza kama sijaona namba za kuingia kwenye kikao. Nilipotazama, nikaona namba hizo na akanishawishi nizitume ili aniruhusu kuingia kwenye kikao,” amesema mchungaji huyo.

“Baada ya kutuma namba hizo, akaunti yangu ya WhatsApp ilizimwa ghafla. Haikupita hata dakika tatu, nikaanza kupokea simu kutoka kwa watu wakiniuliza kwa nini natuma picha za ngono kwenye makundi.”

Lightness Alfred, ambaye mara nyingi hununua bidhaa mtandaoni, amesimulia jinsi akaunti yake ya WhatsApp ilivyodukuliwa na mtu anayedaiwa kuwa Mtanzania.

Mdukuzi huyo alituma ujumbe kwa marafiki wa Lightness, akiomba msaada wa kifedha kwa kudai kuwa ana matatizo.

“Walituma jumbe zilizoandikwa Kiswahili kwa marafiki na makundi mbalimbali. Baadhi ya watu walituma kiasi cha kati ya Sh200,000 na Sh500,000 wakidhani wananisaidia. Ilibidi nianze kusambaza ujumbe kwa kila mtu kwenye orodha yangu kuwaonya wasitume fedha,” amesema Lightness.

Mfanyabiashara ambaye ni mtumiaji wa huduma za shirika moja la ndege la kimataifa, alikumbwa na udanganyifu baada ya kubofya kiungo kilichodaiwa kuwa cha ofa maalumu. Amesema alipobofya kiungo hicho, akaunti yake ya WhatsApp na simu yake vilidukuliwa. “Waliitumia akaunti yangu kutapeli marafiki zangu kwa kuomba fedha na wakaingia mpaka kwenye akaunti yangu ya Facebook,” amesema.

Mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano (IT), Hussein Mfinanga kutoka Kampuni ya PC Point Company Limited ya Dar es Salaam, amesema kutokana na maendeleo ya teknolojia, wadukuaji mahiri hawawezi kukosekana duniani.

Mfinanga amesemamara nyingi wamiliki wa akaunti za WhatsApp au laini za simu hujidhuru wenyewe kwa kufuata maelekezo au kubonyeza viunganishi (links) visivyo salama.

Wimbi hili la sasa la kudukua WhatsApp linafanywa zaidi na wadukuaji kutoka Afrika Magharibi, hasa Nigeria. Ukidukuliwa, mara nyingi namba unayowasiliana nayo ni ya Nigeria, amesema Mfinanga.

Amesema wadukuaji hutumia mbinu ya kudanganya kwa simu, wakidai kuna kikao cha mtandaoni kisha kuomba msomaji kutoa namba ya siri ya kudhibitisha akaunti.

Ukishasoma namba hiyo ya mwisho, WhatsApp yako hupoteza mawasiliano mara moja, amesema Mfinanga.

Emanuel Makumulu, mtaalamu wa IT kutoka Kampuni ya Smart IT Mjini Moshi, amekiri kuwa udukuaji wa akaunti za WhatsApp umekithiri, lakini amesisitiza kuwa bila ushirikiano wa mmiliki, akaunti haiwezi kudukuliwa.

“Kuna namba ya kuthibitisha akaunti mpya ya WhatsApp (code number). Ukimsomea hacker namba hiyo ya tarakimu sita, tayari umempa ufunguo,” amesema Makumulu.

Amesema Tanzania imekuwa shabaha ya wadukuaji kwa sababu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu usalama wa mitandao. Makumulu ameonya dhidi ya kufungua viunganishi (links) visivyo salama, hasa vile ambavyo havina ‘https.’

“Tovuti salama huanza na ‘https’,  ‘s’ inamaanisha usalama. Link isiyo na ‘s’ ni hatari na inapaswa kufutwa mara moja,” amesisitiza Makumulu.

“Tuwe makini na tusitoe code number kwa mtu yeyote. Teknolojia ni nzuri, lakini tuitumie kwa tahadhari,” amesema Makumulu.

Related Posts