Azerbaijan yailazimisha Russia kukiri kudungua ndege yao

Azerbaijan. Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev ameitaka Russia kukubali kuwa ilihusika moja kwa moja katika kuidungua ndege ya Shirika la Ndege la Taifa hilo iliyosababisha vifo vya abiria 38 huku wengine 29 wakinusurika.

Ndege hiyo ya Shirika la Azerbaijan, namba 8432, ilipata ajali Jumatano, Desemba 25, 2024 jijini Aktau, Kazakhstan baada ya kupata changamoto ikiwa kwenye anga la Grozny, Chenchya nchini Russia.

Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria na wahudumu takriban 67 ilikuwa ikitokea jijini Baku nchini Azerbaijani kwenda Grozny, Chechnya nchini Russia, eneo lililotawaliwa na mapigano kati ya vikosi vya Russia dhidi ya Ukraine.

“Tunaweza kutamka wazi kwamba ndege yetu ilidunguliwa na Russia,” Aliyev aliieleza Televisheni ya Taifa ya Azerbaijani.

“Hatusemi kwamba suala hilo lilifanyika kwa kukusudia lakini Russia ndiyo iliyofanya hivyo,” alisisitiza Rais huyo.

Kwa mujibu wa Rais Aliyev, ndege hiyo ilianza kushambuliwa kutokea ardhini na vikosi vya Russia na kumlazimu rubani kuishusha bila kuchukua tahadhari za kuishusha kwa dharura ili kutoleta madhara kwa abiria waliokuweno ndani ya ndege hiyo.

Awali, Ikulu ya Kremlin nchini Russia ilitoa taarifa na kudai kwamba haikuhusika kuidungua ndege hiyo badala yake inaweza kuwa imepata changamoto hiyo kutokana na kuingiliwa na ndegepori katika anga la nchi hiyo.

Msemaji wa Ikulu ya Russia, Dmirty Pescov alisema wakati ndege hiyo inaingia kwenye anga la Russia, mifumo ya kujilinda ya anga la Russia ilikuwa imezimwa japo kulikuwa na mashambulizi ya Droni za Ukraine katika anga la Chechnya nchini humo.

Hata hivyo, Rais Aliyev kwenye mahojiano hayo alienda mbali na kuituhumu Russia kwa kutaka kufunika suala la ndege hiyo kwa siku kadhaa na kusema kitendo cha Russia kutokiri kuhusika na suala hilo siyo cha kiungwana.

Wiki iliyoisha, Mtaalamu wa Masuala ya Anga kutoka Kazakhstan ambaye hakutaka jina lake lifahamike, aliieleza Al Jazeera kuwa: “Hakuna ndegepori wa aina yoyote anayeweza kusababisha madhara makubwa kama ilivyoonekana kwenye mabaki ya ndege hiyo.” Alisisitiza kuwa kusema ndegepori ndiyo chanzo cha ajali hiyo ni uhalifu wa hali ya juu.

Kufuatia madai hayo, Rais wa Russia, Vladimir Putin, Jumamosi Desemba 28, mwaka huu, aliomba msamaha kwa Rais wa Azerbaijan na raia wa taifa hilo kufuatia ajali hiyo aliyoiita ya kusikitisha iliyotokea katika anga la taifa hilo.

Pia, alikiri kwamba mfumo wa kujilinda wa anga wa Russia huenda ulihusika kwa sababu wakati ndege hiyo inaingia kwenye anga la Russia, ndiyo wakati ambao mfumo huo ulikuwa ukikabiliana na mashambulizi ya Droni za Ukraine.

Japo, Ikulu hiyo haikutamka wazi iwapo ndiyo ilihusika kuidungua ndege hiyo, ilisema tayari kesi ya jinai kuhusiana na ajali hiyo imeshafunguliwa nchini humo.

Uamuzi wa Putin kuomba msamaha ulilenga kujibu tamko la Rais Aliyev wa Azerbaijani ambaye aliitaka Russia kujitokeza na kuomba msamaha hadharani kwa kuhusika kwenye ajali hiyo.

“Kwanza, Russia inapaswa kuiomba radhi Azerbaijan. Pili, ikubali kuwa ilihusika, tatu, waliohusika wote wachukuliwe hatua kali na ikubali kulipa fidia kwa waathiriwa wa ajali hiyo wakiwemo waliopata majeraha, waliofariki na familia zao. Na hayo ndiyo masharti yetu kwao,” alisema Rais Aliyev.

Siku mbili baadae, Putin na Aliyev walidaiwa kuzungumza kwa njia ya simu na kusema tayari Jalada la Uchunguzi wa kisa cha ndege hiyo kuanguka limeshafunguliwa kwa kushirikiana na wataalamu wa uchunguzi kutoka nchini Azerbaijan na Kazakhstan.

IMEANDIKWA NA MGONGO KAITIRA KWA MSAADA WA MASHIRIKA

Related Posts