Bosi Jatu aomba mahakama itoe uamuzi upelelezi kutokamilika

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili, likiwemo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa udanganyifu, ameiomba mahakama ifanya uamuzi katika kesi yake kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Saccos ya Jatu kwa madai atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Gasaya ametoa maelezo hayo leo Jumatatu, Desemba 30, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Mshtakiwa ameomba hakimu afanya uamuzi katika kesi hiyo kutokana na kufikisha miaka mitatu akiwa rumande kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Gasaya ametoa maelezo hayo muda mfupi baada ya wakili wa Serikali, Roida Mwakamele kuieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika, hivyo kuomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Gasaya alinyoosha mkono kuashiria kuomba mahakama impe nafasi ya kuzungumza, alipopewa alieleza tarehe iliyopita aliambiwa mahakama itaelezwa upelelezi wake umefikia hatua gani, lakini leo upande wa mashtaka haujaeleza.

Ifuatayo ni sehemu ya malalamiko ya mshtakiwa kwa Hakimu Mhini;

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu, baada ya kuhojiwa na Takukuru siku ile na walipotembelea gerezani upande wa mashtaka (mawakili kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka) waliniambia upelelezi umekamilika, lakini hapa naambiwa bado.

Leo kesi hii inafikisha miaka mitatu nikiwa rumande na upelelezi wake bado haujakamilika.

Hakimu: Ehee, Serikali majibu ya hoja hizi ni yapi?

Wakili: Mheshimiwa hakimu, mimi sina maelezo yoyote zaidi ya kuwa upelelezi wa kesi hii bado haujamilika.

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu naomba mahakama yako ifanye uamuzi.

Hakimu: Mahakama kazi yake ni kusisitiza upelelezi ukamilike kwa haraka, ili iendelee na hatua nyingine.

Mshtakiwa: Basi tarehe ijayo naomba nionane na hakimu mfawidhi wa mahakama hii.

Hakimu: Utapangiwa tarehe ya kuonana naye.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mhini ameahirisha kesi hadi Januari 13, 2025 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.

Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 jijini Dar es Salaam, akiwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, kwa udanganyifu alijipatia Sh 5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo alilojua kuwa sio kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha, tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa alijihusisha na muamala wa Sh 5,139,865,733 kutoka akaunti ya Jatu Saccos iliyopo Benki ya NMB tawi la Temeke kwenda akaunti ya Jatu PLC liyopo Benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Related Posts