Dk Mwinyi ataka wimbo mmoja wa amani, mshikamano 2025

Unguja. Wakati Watanzania leo wakiuaga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano.

Amesema mwaka 2025 ni wa uchaguzi mkuu, hivyo ni wajibu wa viongozi wa kisiasa, taasisi za kijamii, viongozi wa dini na wananchi wote kukumbushana umuhimu wa kudumisha na kuilinda amani ya nchi, kwa lengo kuu moja la maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Katika hotuba yake aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari jana, Dk Mwinyi amesema ni jambo la kujivunia kuona wananchi wanauaga mwaka wakiwa na amani na utulivu huku kukiwa na maendeleo makubwa ambayo Zanzibar imeyapata. 

Rais huyo amesema, itakumbukwa Tanzania inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, tukio alilosema ni la muhimu la kidemokrasia linalowawezesha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.

“Serikali zote mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Tume za Uchaguzi (NEC na ZEC), zimeanza kuchukua hatua za maandalizi ili kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa misingi ya haki na sheria,” amesema Rais Mwinyi.

Rais huyo ametumia fursa ya kuuaga mwaka kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanadumisha amani nchini kabla, wakati, na baada ya uchaguzi,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, kutokana na misingi ya amani, mshikamano na umoja, nchi imepata mafanikio makubwa katika kukuza uchumi, kuimarisha miundombinu, biashara na uwekezaji, huduma za jamii, pamoja na kuimarisha demokrasia na utawala bora.

“Tumepata mafanikio makubwa katika kukuza uchumi kwa kuongeza udhibiti na ukusanyaji wa mapato na kuimarisha uwekezaji na biashara,” amesema Dk Mwinyi.

Aidha, amesema mafanikio makubwa yameonekana katika ujenzi wa barabara mijini na vijijini, viwanja vya ndege na bandari, nyumba za makazi, pamoja na usambazaji wa huduma za umeme na maji safi bila kusahau sekta ya elimu na afya alizosema zimeendelea kuimarishwa karibia Zanzibar nzima.

“Tumefanikiwa kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia programu za utoaji wa mikopo nafuu na kuanzisha masoko ya kisasa ya Mwanakwerekwe na Jumbi,” ameongeza.

Hata hivyo, amewashukuru wananchi, viongozi wa serikali, viongozi wa dini, asasi za kiraia, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha mipango ya maendeleo kwa mwaka unaomalizika wa 2024.

Pia ametoa shukrani maalumu kwa Rais Samia Suluhu Hassan na watendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wao.

“Naomba tuendeleze ushirikiano huu kwa mwaka mpya ili tuzidi kupiga hatua za maendeleo katika kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii yetu,” amesema.

Akizungumzia sekta ya michezo, Dk Mwinyi amesema jitihada kubwa zimefanyika katika kuimarisha sekta ya michezo kwa ukarabati wa viwanja vya Amani Complex na Gombani, sambamba na ujenzi wa viwanja vipya vya michezo.

Amesema jitihada hizo zinalenga kuimarisha sekta ya michezo na kuchochea utalii kupitia matamasha na mashindano ya kimataifa.

Hivyo, amesema Serikali inalenga kuwa na miundombinu inayokidhi mahitaji ya mashindano ya CHAN kwa mwaka 2025 na Afcon mwaka 2027, yatakayoshirikisha Tanzania, Kenya na Uganda.

Kutokana na umuhimu wa Mapinduzi ya mwaka 1964, Dk Mwinyi amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika sherehe za miaka 61 ya Mapinduzi Januari 12, 2025.

Matukio hayo yatashirikisha uzinduzi wa miradi ya maendeleo, uwekaji wa mawe ya msingi, michezo, na shughuli za kitamaduni. Sherehe hizi zitafikia kilele chake Januari 12, 2025, katika Uwanja wa Gombani, Pemba.

“Sherehe hizi ni zetu sote, hivyo nawakaribisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kuzifanikisha,” amesema.

Tunapouaga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2025, tunao wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kudumisha amani, mshikamano, na umoja wa kitaifa katika nchi yetu.

Related Posts