Moshi. Wakati mamia ya wananchi wa kabila la Wachaga wakiendelea kukukutana kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka katika kijiji cha Umbwe Sinde, Kata ya Kibosho Magharibi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka amewataka wananchi kuachana na tabia ya kuficha maovu na kutumia jani la ‘sale’ kama kisingizio cha kuombana msamaha.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, leo Jumatatu, Desemba 30, 2024 katika mkutano uliohudhuriwa na zaidi ya wananchi 400 wa kikundi cha Umbwe Sinde Community kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki la Umbwe, Dk Timbuka amesema tabia hiyo inachochea matukio ya ukatili katika familia na haikubaliki katika jamii.
Amesisitiza kutumia jani la ‘sale’ kama njia ya kuombana msamaha katika matukio ya ubakaji, ulawiti na hata mauaji, kunatoa mwanya kwa vitendo hivyo kuendelea kufanyika.
Hivyo, amewataka wananchi kuacha tabia hiyo na kuruhusu sheria kuchukua mkondo wake.
“Tushirikiane na Serikali kuwafichua wote wanaofanya vitendo vya uvunjifu wa amani. Tusifumbie macho uovu au kuficha wahalifu katika maeneo yetu.
“Inapotokea mtoto amebakwa au kulawitiwa, wazazi hukutana kuombana msamaha, lakini ukweli ni kwamba anayepaswa kuombwa msamaha ni mtoto, si mzazi. Hili si sahihi na tunapaswa kubadilika,” Amesema.
Dk Timbuka amesema desturi ya kutumia ‘sale’ ni ya kizamani na haipaswi kuendelea, huku akisisitiza sheria inapaswa kufuata mkondo wake ili kuhakikisha jamii inakuwa salama.
Kuhusu wazo la kujenga kituo cha polisi kijijini Umbwe, Dk Timbuka amelipongeza na kusema Serikali inaunga mkono mpango huo na kwamba Serikali itashirikiana na wananchi kuhakikisha mradi huo unakamilika mapema.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa kikundi cha Umbwe Sinde Community, Sisti Massawe amesema mkutano wao wa mwisho wa mwaka umekuwa fursa ya kujadili changamoto zinazowakabili.
Amesema wameona kuna umuhimu wa kuanzisha mchakato wa kujenga kituo hicho cha polisi kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama.
“Umbali wa kilomita 18 kwenda na kurudi hadi kituo cha polisi, pamoja na gharama ya zaidi ya Sh9,000 kwa usafiri wa bodaboda ni changamoto kubwa kwa wananchi, ndiyo maana tumeamua kuanzisha mchakato wa ujenzi wa kituo hicho mapema Januari mwakani,” amesema Massawe.
Amesema ukosefu wa kituo cha polisi umechangia kushamiri kwa matukio ya ukatili na kuongeza kuwa vijana wengi hawana ajira rasmi, jambo ambalo linalochangia matatizo ya kijamii.
Kwa upande wake, Padri Andrew Massawe, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, amesema mpango wa kujenga kituo cha polisi utapunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya ukatili na kuimarisha usalama wa kijiji.
Amesisitiza kuwa mshikamano wa jamii utasaidia kufanikisha mradi huo na kuboresha maisha ya wakazi wa Umbwe Sinde na maeneo ya jirani.