DKT. DIMWA AZUNGUMZIA UIMARISHAJI SEKTA YA AFYA NCHINI.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amesema chama hicho kimeendelea kutafsiri kwa vitendo sera zake za uimarishaji wa huduma za afya nchini zinazoendana na mahitaji ya wananchi wa makundi yote.

Hayo ameyasema katika ziara yake ya kuwatembelea wagonjwa na watu wenye mahitaji maalum katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mjini Unguja. Dkt. Dimwa alisema lengo la ziara hiyo ni kuwajulia hali zao ili kuwapa faraja na matumaini ya kuishi kwa kujiamini kama walivyo watu wengine.

Katika maelezo yake akisisitiza kwamba CCM inatambua umuhimu wa kuwa karibu na wananchi ambao ndio wanaotoa ridhaa kwa serikali zilizopo madarakani. “Napata faraja kubwa ninapowatembelea waajiri wangu ambao ndio nyinyi mliotupa kazi ya kuongoza Chama na Serikali zake, hivyo kuja kwenu sio tu sehemu ya kutembea bali ni kubadilishana mawazo juu ya hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na serikali yetu na chama kwa ujumla,” alisema Dkt. Dimwa.

Katika ziara hiyo, Dkt. Dimwa alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kusimamia kwa ufanisi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iendelee kuweka mazingira bora ya huduma za afya na sekta zingine za kijamii na kiuchumi.

Alisema, CCM inatilia mkazo katika kuimarisha miundombinu ya afya, na kwamba Serikali imejizatiti kuleta vifaa tiba vya kisasa katika kila hospitali, hivyo wananchi wataendelea kupata huduma bora za afya.

Aidha, Dkt. Dimwa aliongeza kuwa Serikali ya CCM imeendelea kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kwa kuboresha mazingira yao ili waweze kufanya kazi zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Alisema kuwa chama cha Mapinduzi kimekuwa ni daraja muhimu linalowaunganisha wananchi na Serikali yao katika juhudi za kuimarisha miundombinu ya kijamii, hivyo kila mtu, bila kujali hali yake, anapata fursa ya kuishi kwa hadhi na kujiamini.

Kupitia ziara hiyo aliwatembelea wagonjwa, wazee wa CCM na watu wenye mahitaji maalum, wakiwemo Katibu wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar aliyelazwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja Haji Machano Haji, Diwani Mstaafu wa CCM Ameir Makungu nyumbani kwake Rahaleo pamoja na Aisha Abdalla Haji ambaye ni mwanachama wa CCM mwenye mahitaji maalum huko nyumbani kwao Kwahani.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Katibu wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar ndugu Haji Machano Haji anayepatiwa matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa,akizungumza na kumkabidhi kiti mwendo (wheelchair) kwa ajili ya usafiri ndugu Aisha Abdalla Haji (wa pili kulia) ambaye ni mtu mwenye ulemavu.

Related Posts