KIUNGO wa Azam FC, Feisal Salum amekata mzizi fitna kuhusu maneno yanayoendelea kusemwa kwamba huenda akatimikia Simba, akifunguka kuwa kama ataondoka anapocheza sasa basi hawezi kujiunga na timu yoyote Bongo ikiwamo ya Wekundu wa Msimbazi.
Fei ambaye aliwahi kuichezea Yanga kwa mafanikio, ameendeleza moto wake hadi alipojiunga na Azam ambako alisaini mkataba wa miaka mitatu ambao unaisha msimu ujao.
Kiungo huyo wa boli ameendelea kufanya vizuri ndani ya ligi baada ya msimu uliopita kumaliza akiwa nafasi ya pili kwa mabao 19, na tayari msimu huu amehusika katika mabao 13, akifunga manne na kutoa asisti 9.
Akizungumza na Mwanaspoti Fei alisema kuwa, endapo ataondoka Azam hawezi kujiunga na timu yoyote ya ndani kwa sasa ikiwamo Simba ambayo inatajwa sana kuwa atatimkia huko wakati wowote.
Alisema kuwa, akili yake kwa sasa ni kutafuta timu ya kwenda kucheza njeya nchi ili akaongeze kipaji chake na sio ndani kwani tayari ameshafanikiwa kujijenga katika ligi ya nyumbani.
“Sasa nipo Azam nina amani kubwa lakini pia nimecheza Yanga na kupata mafanikio makubwa kwa hiyo kitu kilichosalia kwangu ni kwenda kucheza nje.
“Natamani nije kuongeza kitu kwenye timu ya Taifa, naamini pia Azam haitanizuia kama timu zitakuja kwa nia ya kunitaka, hivyo ninachokitamani zaidi ni changamoto mpya.”
Mwanaspoti iliwahi kuripoti,”Miamba ya soka ya Afrika Kusini, Kaizer Chiefs imeonyesha dhamira ya kuvunja mfumo wake wa malipo ili kumsajili kiungo wa kati wa kimataifa wa Tanzania, Feisal Salum katika dirisha dogo la usajili la Januari, mwakani.
Taarifa hiyo iliongeza: Azam wanapambana kumbakiza kiungo huyo muhimu kwa kumpa mkataba mpya wenye mshahara mkubwa zaidi, lakini vita ya usajili imechukua sura mpya baada ya Simba na Chiefs kuonyesha nia kubwa ya kumnasa.
Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen la huko Afrika Kusini, Chiefs wapo tayari kutumia kiasi kikubwa cha fedha ili kuhakikisha mchezaji huyo anajiunga na kikosi chao.
Hii inajumuisha ofa bora zaidi kuliko kile ambacho Azam au Simba wanaweza kutoa. Hata hivyo, kuondoka kwa Feisal Tanzania itategemea na mafanikio ya mazungumzo ya pande husika.
Aliyekuwa kocha wa Mamelodi Sundowns, Rulani Mokwena aliwahi kuonyesha kuvutiwa na kiungo huyo, wakati Azam ilipokwenda pre-season nchini Afrika Kusini.
Kama itatokea timu itakayofika dau zuri zaidi na Azam kipindi hiki ambacho ana mkataba na klabu hiyo, basi huenda Fei akasepa kuzifuata ndoto zake.