Jinsi Kansela Olaf Scholz alivyopoteza umaarufu wake – DW – 28.12.2024

Mnamo Septemba, Scholz alikwepa swali la mwandishi wa habari kuhusu urithi wake kisiasa. “Nadhani mtu anapaswa kuwa makini na wanasiasa wanaofikiria kuhusu hilo kabla ya muhula wao kuisha,” alisema katika mahojiano na gazeti la Tagesspiegel la Berlin.

Lakini baada ya kuvunjika kwa muungano wake wa vyama vitatu vya mrengo wa kati-kushoto, Scholz anaweza kuwa ameanza kujiuliza swali hilo.

Ingawa uongozi wa SPD bado unamuunga mkono rasmi kuwa mgombea wao mkuu kwa uchaguzi wa Februari 23, 2025, wito ndani ya chama umeibuka wa kumbadilisha Scholz na Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius, mwenye umri wa miaka 64, ambaye amekuwa mwanasiasa maarufu zaidi nchini Ujerumani kwa miezi kadhaa kulingana na kura za maoni.

Ikiwa, kama inavyotarajiwa, muungano wa vyama vya mrengo wa kulia wa CDU na CSU utaongoza nafasi ya ukansela, Scholz atakuwa na muda mfupi zaidi wa uongozi miongoni mwa wakansela wanne wa SPD katika historia ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.

Berlin 2024 | Olaf Scholz kabla ya taarifa ya serikali katika Bundestag
Kwenye kura za maoni, Waziri wa Ulinzi wa SPD Boris Pistorius (nyuma) ni maarufu zaidi kuliko Olaf Scholz (mbele).Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Changamoto za umaarufu mdogo

Scholz ameonyesha dhamira ya kushinda, licha ya changamoto kubwa zinazokikabili chama chake cha SPD ambacho kiko nyuma sana kwenye kura za maoni ikilinganishwa na CDU/CSU. Scholz hajawahi kukosa kujiamini, hata katika hali zinazoonekana kukosa matumaini. Wakosoaji wake wamemshutumu kwa kuwa na mtazamo uliopotoka wa hali halisi, wakisema kuwa anaishi katika “ulimwengu wake mwenyewe.”

Soma pia: Steinmeier alivunja bunge na kupisha njia ya uchaguzi wa mapema

Kiongozi wa CDU, Friedrich Merz, alikosoa hotuba ya Scholz bungeni baada ya kuvunjika kwa muungano wake, akisema, “Wewe huwezi kuelewa kinachoendelea huko nje nchini kwa sasa.”

Serikali isiyopendwa zaidi baada ya vita

Utawala wa Scholz umekumbwa na changamoto nyingi, kuanzia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine hadi mzozo wa nishati, mfumuko wa bei, mdororo wa uchumi, na mvutano wa hifadhi ya wakimbizi barani Ulaya. Zaidi ya hayo, mafanikio makubwa ya kisiasa ya mrengo wa kulia baada ya Vita vya Pili vya Dunia yameathiri serikali yake.

Scholz achukua usukani kutoka kwa Merkel kama kansela wa Ujerumani

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Muungano wa “taa za trafiki,” ulioundwa na SPD, FDP (waliberali), na Kijani (wanamazingira), ulianza kama muungano wa maendeleo baada ya uchaguzi wa 2021. Hata hivyo, tofauti kati ya programu za vyama hivi zilionekana kuwa kubwa mno, na miezi ya mabishano ya hadharani ilisababisha muungano huo kuwa serikali isiyopendwa zaidi nchini Ujerumani tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Scholz, hata hivyo, anaendelea kuwa na matumaini. Anakumbusha jinsi alivyoongoza SPD kushinda uchaguzi wa 2021 licha ya kuwa nyuma kwenye kura za maoni miezi mitatu kabla ya uchaguzi huo.

Scholzomat: Sifa ya kiongozi roboti

Ushindi wa 2021 ulikuwa kilele cha taaluma ya Scholz ya miongo kadhaa kisiasa. Alijiunga na SPD akiwa mwanafunzi mwaka 1975 na baadaye aliwahi kuwa mwanasheria na mbunge wa Hamburg. Alihudumu kama Waziri wa Kazi katika muungano wa kwanza wa vyama vikuu chini ya Angela Merkel na baadaye kama Meya wa Hamburg.

Soma pia: Ujerumani yajiandaa kwa uchaguzi baada ya Scholz kupoteza kura ya imani

Mwaka 2002, Scholz alipata jina la utani “Scholzomat,” mchanganyiko wa “Scholz” na “Automat,” ikimaanisha mtindo wake wa kitaalamu lakini wa urasimu wa kuzungumza kana kwamba ni mashine. Sifa hii ilimfuata hadi  kwenye nafasi yake ya Kansela, ambapo ukimya wake wakati wa migogoro mikubwa umeelezwa kama kujitenga na watu.

Olaf Scholz katika kongamano la shirikisho la Juso mnamo 1984
Scholz alitoa mchango mkubwa katika shirika la vijana la SPD katika miaka ya 1980Picha: Gladstone/Wikipedia

Hata baada ya wafuasi wake kumtaka abadilishe mtindo wake na kuwa mwenye mawasiliano zaidi, Scholz amekataa kubadilika. Wakosoaji wanasema ametumia muda mwingi kutegemea ufanisi wake wa kiutendaji kuliko kushirikiana na wananchi kwa hisia.

Mustakabali wa Scholz

Ingawa uongozi wa SPD umemuunga mkono rasmi Scholz kama mgombea wao mkuu, uteuzi rasmi unatarajiwa kufanyika katika mkutano wa chama Januari. Ikiwa Scholz atashinda uchaguzi wa 2025, itakuwa ushindi wa kushangaza, lakini historia ya kisiasa ya Scholz inaonyesha kuwa mara nyingi amefanikiwa kupita matarajio ya wengi.

Related Posts