Jinsi ya kuepuka kupigwa na radi

Dar es Salaam. Kutokaa chini ya miti, kutembea peku katika maji na kusimama katika nguzo ndefu za chuma vimetajwa kuwa vitu visivyopaswa kufanywa na mtu wakati mvua ikinyesha ili asipigwe na radi.

Tahadhari hiyo imetolewa na mtaalamu kutoka Ofisi Kuu ya Utabiri kutoka Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA), alipozungumza na Mwananchi.

Ametoa tahadhari hiyo wakati ambao Mwananchi imeripoti watu watano wa familia moja kutoka jamii ya wafugaji kupoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa, baada ya kupigwa na radi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku.

Tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Isangawane, Kata ya Matwiga, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya na inaelezwa hilo ni tukio la pili kwa mwezi huu. Awali radi iliyotokea iliua mtu mmoja.

Katika tukio la Desemba 29, 2024 waliopoteza maisha ni Balaa Scania (28), Masele Masiganya (16), Hemi Tati (10), Manangu Ngwisa (18) na Kulwa Lawaje(10), huku waliojeruhiwa wakiwa ni Manyenge Masagala (13), Serusi Solo (13), Paskalia Kalez (16), Gulu Scania (30) na Huruma Kalezi (19).

Akizungumza namna mtu anavyoweza kujilinda, Meneja Ofisi Kuu ya Utabiri TMA, Kantamla Mafuru amesema umeme wa radi unaposafiri kutoka wenye wingu kuja chini (ardhini) ukikutana na kitu ambacho ni nyenzo nzuri inayoweza kutumika kusafirisha umeme huo hupitia hapo.

Amesema hali hiyo hufanya mtu au mfugo anayepita au yupo karibu na kisafirisha umeme huo kupata madhara.

“Kitu kirefu ambacho kinaweza kusafirisha hiyo chaji inaweza kuwa mti mrefu mbichi, ukikaa karibu na mti mrefu utapigwa na radi. Ukikaa karibu na chuma kirefu ile chaji itakufanya upate madhara,” amesema Mafuru.

Amesema pia kama kuna maji katika eneo la wazi na mtu aliyepo katika maji hayo hajavaa ndala au viatu, umeme wa radi unaposhuka chini ukipiga kwenye maji mtu aliyepo katika eneo hilo lazima ataathirika.

Akizungumzia watu ambao mvua inawakuta katikati ya msitu wenye miti mingi, amewataka kutafuta sehemu ambazo hazina miti.

“Sasa wakiwa sehemu ambayo haina miti wanachopaswa kufanya si kusimama, bali wachuchumae na vichwa wainamishe chini ili radi inapokuja isiaathiri,” amesema Mafuru.

Pia amewataka wananchi kuwa na tabia ya kukaa ndani pindi mvua inaponyesha, badala ya kufanya shughuli mbalimbali katika mvua ili kujiepusha na madhara hayo.

Mtaalamu na mchambuzi wa hali ya hewa kutoka TMA, Rose Senyagwa aliliambia Mwananchi Mei mwaka huu kuwa radi ni umeme unaotoka katika wingu linalojulikana kama wingu ng’amba.

Alifafanua kuwa aina hiyo ya wingu kwa kawaida hufanyika baada ya jua kali kupiga katika ardhi yenye unyevunyevu wa kutosha au vyanzo vya maji kama bahari, mito na maziwa.

“Kiasi kikubwa cha unyevunyevu huvukizwa (mvuke) na kusafirishwa angani, na kutengeneza wingu zito lenye barafu ndani yake lijulikanalo kama wingu ng’amba.

“Wingu hili likiwa na uzito wa kutosha, mvua kubwa huanza kunyesha. Wingu hili pia hutoa chaji za umeme wakati mabarafu ndani ya mawingu yakigongana angani,” alisema Rose na kuongeza chaji hizo zinaweza kusafiri kutoka kwenye wingu moja hadi linguine au zikaenda juu zaidi angani au zikatoka kwenye wingu hadi ardhini.

Aliendelea kueleza kuwa chaji zinazosafiri kuja ardhini ndizo huleta madhara makubwa na zinapokutana na kitu chochote mfano, miti, minara, wanyama, binadamu husababisha madhara, ikiwemo vifo.

“Kwa kawaida chaji hizi hufuata vitu virefu kama miti mirefu au minara. Kunapokuwa na radi tunashauriwa kuepuka kukaa chini ya miti, minara mirefu,” alisema.

Ili kujikinga na madhara yake, Rose alisema unapaswa kuepuka kutumia vitu kama simu au vitu vya kielektroniki wakati wa radi.

Katika matukio tofauti yaliyowahi kuripotiwa na Mwananchi miongoni mwake ni lile la ng’ombe 22 kufa baada ya kupigwa na radi Desemba 9, 2024. Tukio hilo lilitokea Kijiji cha Songambele Azimio, Kata ya Msanda Muungano wilayani Sumbawanga Mkoa wa Rukwa.

Tukio lingine ni mkazi mmoja wa Kitongoji cha Uvihangani Kata ya Marui, Wilaya ya Kisarawe, Suna Mpongoja ambaye alifariki dunia baada ya kupigwa na radi akiwa anakinga maji pembezoni mwa msingi wa nyumba yake Machi 15, mwaka huu.

Pia Januari 23, mwaka huu, Mwananchi iliripoti taarifa ya mkazi wa Kijiji cha Mtimbwilimbwi katika Halmashauri ya Mji Nanyamba, mkoani Mtwara, Dadi Linyata kufariki dunia kwa kupigwa na radi akitokea mazikoni, huku wengine wanne wakijeruhiwa.

Related Posts