SIKU moja baada ya kutangaza kikosi cha wachezaji 28 kinachoingia kambini kwa ajili ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kocha Ahmed Ally amesema ni heshima kwake kukabidhiwa majukumu hayo huku akianika mikakati yake.
Ahmed ambaye anainoa JKT Tanzania ameteuliwa kuiongoza Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kushiriki michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Januari 3 hadi 13, 2025 visiwani Pemba.
Timu sita za taifa zitashiriki ambazo ni wenyeji Zanzibar Heroes, Kilimanjaro Stars, Burundi, Burkina Faso, Kenya na Uganda.
“Ni nafasi nzuri nimeipata, nawashukuru viongozi kwa kuona kitu kutoka kwangu, sasa ni nafasi ya mimi kuendelea kuboresha uwezo wangu kwani hii ni mara ya kwanza kuongoza timu ya taifa.
“Baada ya kupewa majukumu haya nimekaa na wenzangu na kuita kikosi ambacho tunaamini ni imara kitakachofanya vizuri katika mashindano hayo na baadaye kikatumika kuunda timu ya wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan) na Afcon,” alisema.
Akizungumzia wachezaji aliowaita, alisema wamezingatia hasa wachezaji ambao wamekuwa wakiitwa mara kwa mara na hawapati nafasi ya kucheza lengo ni kuboresha uwezo wao na pia kuandaa wachezaji wengine bora kwa ajili ya michuano iliyo mbele yao.
“Tanzania inatarajiwa kuwa nchi mwenyeji wa mashindano ya Chan hivyo maandalizi ya wachezaji yanaanza na michuano tunayoshiriki sasa. Naamini wachezaji waliopata nafasi watafanya kazi nzuri ili kujihakikishia nafasi,” alisema kocha huyo.
Wachezaji walioitwa kuunda kikosi hicho ni Metacha Mnata (Singida Black Stars), Ramadhani Chalamanda (Kagera Sugar), Anthony Mpemba (Azam FC, Ngorongoro Heroes), Lusajo Mwaikenda (Azam FC), Nickson Mosha (KMC FC, Ngorongoro Heroes), Vedastus Masinde (TMA STARS, Ngorongoro Heroes) na Lameck Lawi (Coastal Union, Ngorongoro Heroes).
Wengine ni Wilson Nangu (JKT Tanzania), David Bryson (JKT Tanzania), Pascal Msindo (Azam FC), Hijjah Shamte (Kagera Sugar, Ngorongoro Heroes), Semfuko Charles (Coastal Union), Said Naushad (Kagera Sugar), Ahmed Bakari (KMC, Ngorongoro Heroes) na Sospeter Bajana (Azam FC).
Pia wapo Abdulkarim Kiswanya (Azam FC, Ngorongoro Heroes), Idd Nado (Azam FC), Bakary Msimu (Coastal Union, Ngorongoro Heroes) Zidane Sereri (Dodoma Jiji, Ngorongoro Heroes), Ayoub Lyanga (Singida Black Stars), Nassoro Saadun (Azam FC), Offen Chikola (KenGold), Joshua Ibrahim (KenGold), Abdul Hamis (Azam FC), Sabri Kondo (KVZ, Ngorongoro Heroes), Gamba Idd (JKT Tanzania) na Crispin Ngushi (Mashujaa).