Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amewataka Maafisa na Wapiganaji wa Vikosi vya SMZ kuwa wazalendo, kufanya kazi kwa kufuata maadili na kusimamia haki na uwadilifu kwa wanaowaongoza.
Ameyasema hayo wakati akizindua Jengo la Makao Makuu ya Chuo cha Mafunzo Kilimani Mjini Unguja ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais amewataka Maafisa na wapiganaji wa Vikosi vya SMZ kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yao na kuzitumia vyema rasilimali wanazopatiwa hasa katika ujenzi wa miradi mbali mbali ya Serikali na Taasisi Binafsi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kuzidi kuaminika ndani na nje ya nchi.
Amesema Idara ya Chuo cha Mafunzo imefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa miradi mbali mbali ambayo wamepatiwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivyo amemtaka Kamishna wa chuo hicho kuwaenzi mafundi wa idara hio ili kuweza kuwapa motisha katika kulitumika Taifa.
Aidha Mhe. Hemed amesema Nidhamu na uwajibikaji ndani na nje ya maeneo yao ya kazi ndio msingi mkubwa wa mafanikio utakao wajengea heshima wao na Taifa kwa ujumla.
Sambamba na ahayo Makamu wa Pili wa Rais amewataka viongozi kuhakikisha wanaacha alama chanya katika maeneo yao wanayofanyia kazi ili uwepo wao uendelee kudumu hata baada ya kustafu jambo ambalo ni heshima kwao na kwa Nchi wanayoitumikia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Massoud Ali Mohamed amesema Serikali inajipanga kujenga chuo kikubwa cha kisasa cha Mafunzo katika eneo la Hanyegwa Mchana ili kuimarisha mfumo wa haki jinai na kurahisisha mifumo ya utendaji wa Kazi kwa Maafisa na wapiganaji wa Chuo cha mafunzo.
Mhe. Massoud amesema ni wajibu wa Maafisa na wapiganaji wa vikosi vyote vya SMZ kutanguliza maslahi ya Taifa mbele kwa kuwa tayari kuipigania nchi hasa katika harakati za kimaendeleo ili kutimiza dhamira njema ya Mhe.Rais Dkt. Mwinyi ya kuifungua Zanzibar Kiuchumi na Kimaendeleo.
Massoud amewataka Maafisa na Wapiganaji wa vikosi vyote vya SMZ kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Taasisi nyengine pamoja na kudumisha nidhamu na uwajibikaji ndani na nje ya kazi ili kulinda hadhi na heshima ya Idara Maalum za SMZ.
Akisoma taarifa ya kitalamu juu ya ujenzi wa Makao makuu ya chuo cha mafunzoo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Ndugu Issa Mahfoudh Haji amesena kufuatia changamoto iliyokuwa ikiwakabili Maafisa na wapiganaji wa chuo cha mafunzo ya kukosa ofisi rasmi za kufanyia kazi, Wizara iliamua kujenga ofii ya kisasa itakayozikusanya pamoja Ofisi zote zinazo simamia na jeshi hilo.
Amesema ujenzi wa Ofisi hizo ni muhimu kwa Maafisa na wapiganaji wa chuo cha Mafunzo hasa katika utendeji kazi wa kikosi hicho pamoja na kuzienzi fikra na falsafa za waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Amefahamisha kuwa mradi wa ujenzi wa ofisi hizo hadi kumalizika kwake unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 30 ziliztolewa na Serikali ya Mapinduzi ya zanzibar uliojumuisha vyumba vya ofisi 30, kumbi mbili za mikutano na vyoo kwa ajili ya Maafisa na wapiganaji wa jeshi hilo jambo litakaloongeza ufanisi kwa watendaji hao.
Mapema Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar Ngudu. KHAMIS BAKARI KHAMIS ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Zanzibar pamoja na kuwawekea mazingira mazuri Askari na Maafisa wa Vikosi vya SMZ ili kuimarisha utendaji wao wa kazi.
Kamishna Khamis amesema ujenzi wa Jengo hilo umetumia fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuahidi kuwa kwa kushirikiana na Maafisa na Askari wa Chuo cha Mafunzo watahakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa bidiii na kwa uweledi pamoja na kuimariasha amani na utulivu uliopo nchini.