Majogoro ashtukia jambo Sauzi | Mwanaspoti

KIUNGO wa Chippa United ya Afrika Kusini, Baraka Majogoro amesema unapocheza na timu kubwa kama Mamelodi Sundowns maandalizi yake yanakuwa tofauti.

Mtanzania huyo ni msimu wake wa pili kucheza Afrika Kusini akisajiliwa mwaka jana akitokea KMC.

Chippa United iko nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi hiyo inayoongozwa na Mamelodi kwenye mechi 10 ikishinda nne, sare mbili na kupoteza nne ikikusanya pointi 14.

Akizungumza na Mwanaspoti, Majogoro alisema kwenye mechi ngumu kama hizo unahitaji utimamu wa mwili na akili hivyo maandalizi yake yanakuwa makubwa.

“Ni kweli timu kubwa kama unavyo sema ila hakuna maandalizi madogo ukiwa unajiandaa kwenye mechi na bingwa kwani hakuna vita ndogo au vita unayohitaji maandalizi madogo ya kiakili na mwili,” alisema.

Kuhusu kucheza na Mtanzania mwenzake, Gadiel Michael kwenye timu moja alisema: “Nafurahi kuona niko nafanya kazi nje ya nyumbani na Mtanzania mwenzangu hivyo tunaweza kubadilishana mawazo na kuongea lugha moja na kuelewana na kusikilizana.”

Related Posts