Maswi amzungumzia Jaji Werema, akumbuka Escrow

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi amemtaja Mwanasheria Mkuu (AG) mstaafu, Jaji Frederick Werema kuwa mmoja wa viongozi waliokuwa na misimamo huku akikumbusha weledi aliouonyesha wakati wa sakata la akaunti ya Escrow.

Kauli ya Maswi inakuja saa chache baada ya taarifa ya kifo cha Jaji Werema kilichotokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo mchana.

Taarifa ya kifo cha Jaji Werema imethibitishwa na Katibu wa Halmashauri ya Walei, Parokia ya Mtakatibu Martha Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Salome Ntaro.

Kwa mujibu wa taarifa ya Salome, Jaji Werema (aliyekuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei ya Parokia hiyo) amefariki dunia mchana wa leo, Jumatatu Desemba 30, 2024 na taratibu zinaendelea kupangwa na umma utajulishwa.

“Kwa masikitiko makubwa, nimepokea taarifa ya kifo cha mwenyekiti wetu wa Parokia ya Martha Judge na Mwanasheria Mkuu mstaafu, mzee wetu Frederick Werema kilichotokea mchana wa leo katika Hospital ya Muhimbili,” ameeleza Salome katika taarifa hiyo.

Hata hivyo, Maswi na Jaji Werema wana historia katika utumishi wa umma. Wawili hao mwaka 2014 walituhumiwa pamoja kuhusika na uchotaji fedha zaidi ya Sh200 bilioni kutoka akaunti ya Escrow.

Maswi wakati huo, akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Jaji Werema Mwanasheria Mkuu, walituhumiwa sambamba na mawaziri kadhaa.

Kutokana na hayo, Maswi alisimamishwa kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete wakati huo, kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake, huku Jaji Werema na mawaziri kadhaa wakijiuzulu.

Akizungumza na Mwananchi leo kuhusu anavyomkumbuka Jaji Werema, Katibu Mkuu huyo anayehudumu Wizara ya Katiba na Sheria kwa sasa, amesema anamkumbuka kama mtu aliyekuwa na msimamo na alisimamia anachokiamini.

Si msimamo pekee, amesema isingekuwa rahisi kuhoji uadilifu wa Jaji Werema na kwamba ni miongoni mwa viongozi aliowahi kuwaheshimu kwa misimamo yao.

“Unakumbuka hata kipindi kile wakati wananihojihoji na kunisemasema, aliwaambia muacheni Maswi niulizeni mimi. Ni watu wangapi wenye weledi na uthubutu wa kusema hivyo,” amesema Maswi.

Amesisitiza Taifa limepoteza kiongozi mahiri na atabaki kuwa historia nzuri kwa vizazi vijavyo kutokana na ufanisi wake katika utendaji.

Kwa upande wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi naye ameiambia Mwananchi kuwa ingawa Jaji Werema amefariki dunia, lakini atabaki kuwa mmoja kati ya watu walioitendea vema taaluma ya uwakili.

Kauli hiyo inatokana na kile alichokifafanua, AG huyo mstaafu kuwa,  hakuwa na hofu ya kusimamia alichokiamini kuwa ni sahihi bila kujali mitazamo ya wengine.

“Ni mtu bora aliyekuwa na wivu na taaluma yake na hakuwa na hofu ya kusimamia alichokiamini ni sahihi bila kujali wengine walikuwa na mtazamo gani,” amesema Mwabukusi.

Akizungumzia utendaji na uadilifu wake, Mwabukusi amesema ulimfanya awe mmoja wa mawakili walioonyesha ukomavu kitaaluma, kwa kuwa hakuwa anayumbishwa kwa mashinikizo bali alisimamia alichokiamini na alikitetea.

Akizungumzia msiba huo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Eliezer Feleshi amesema amefanya kazi na Jaji Werema kwa muda mrefu tangu walipoajiriwa kuwa mawakili wa Serikali.

Amesema wamekuwa wakikutana katika nafasi tofauti lakini zote ndani ya ulingo wa sheria, wakishirikiana kutekeleza majukumu, huku akimtaja kuwa mmoja ya viongozi waliokuwa na weledi.

Mbali na ushirikiano walipokuwa watumishi wa umma, amesema aliendelea kushirikiana na Jaji Werema hata alipostaafu, hasa akimwomba ushauri katika nyadhifa alizomrithi.

“Yeye alikuwa Jaji na mimi niliteuliwa kuwa Jaji, yeye alikuwa AG na mimi niliteuliwa kuwa AG kwa hiyo nilikutana naye na kuwasiliana naye kwa simu mara kwa mara kushauriana mambo mbalimbali,” amesema.

Kwa mujibu wa Jaji Feleshi, alipokuwa AG alizindua Chama cha Wanasheria wa Serikali, Jaji Werema na Andrew Chenge ni miongoni mwa wanasheria wakuu wastaafu waliohudhuria na kutoa muhadhara.

“Jaji Werema ni mtu aliyelitumikia Taifa kwa weledi kwa sababu tuliofanya kazi za kisheria katika nyanja mtambuka tunaelewa vitu alivyopigania akiwa wakili, Jaji na AG,” amesema.

Mbali na ubobezi katika taaluma ya sheria unaojulikana na wengi, Jaji Werema amewahi kuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert jijini Dar es Salaam tangu 1979 hadi 1980.

Sambamba na nafasi hiyo, pia amekuwa Wakili tangu mwaka 1984 hadi 2006 na baadaye 2009 aliteuliwa kuwa AG, nafasi aliyohudumu hadi mwaka 2014 alipojiuzulu.

Pia, amewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu katika Divisheni ya Biashara na amefariki akiwa na umri wa miaka 69, alizaliwa Oktoba mwaka 1955.

Hadi anafariki alikuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya binafsi ya huduma za kisheria ya FMD.

Related Posts