Mzee Mechili asimulia safari ya miaka 75 ya ndoa

Moshi. Taasisi ya ndoa imekuwa ikikumbwa na changamoto nyingi katika miaka ya hivi karibuni, hali inayosababisha ndoa nyingi kuvunjika mapema.

Hata hivyo, Mzee Joseph Mechili (95) na mkewe Alphonsina Mechili (92) ambao wamefanikiwa kufanikisha safari yao ya ndoa kwa miaka 75 sasa na kuvivuka vikwazo mbalimbali.

Mwananchi Digital imefika nyumbani kwa wazee hao jana, Desemba 29, 2024 kushuhudia ibada ya kumshukuru Mungu iliyoambana na sherehe ya Jubilei ya miaka 75 ya ndoa yao. Ibada hiyo iliongozwa na mtoto wao, Padri John Joseph na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Akihubiri kwenye ibada hiyo, Padri John amesema wanandoa kuadhimisha Jubilei ya miaka 75 si jambo la kawaida katika dunia ya sasa.

“Wanafanya Jubilei ambayo haipatikani kwa urahisi na wana afya nzuri. Ukiwaangalia wameng’ang’ania katika upendo wa Yesu, lakini kumpenda Mungu na wao kupendana, tunawapongeza sana, hawa wazee si kwamba hajapitia mabonde na milima, lakini kuvumiliana, kuchukuliana na kupendana kwa dhati, kumewafikisha hapa walipo. Hongereni sana,” amesema Padri John.

Joseph asimulia miaka 75 ya ndoa yake

Akizungumza katika sherehe hiyo, mzee Joseph ambaye muda wote alionekana mwenye furaha, anasema katika maisha yao ya ndoa wamekuwa wakipendana sana na mkewe Alphonsina.

“Huyu mke wangu nilikutana naye akiwa anaishi hapa jirani kwa ndugu yake. Wakati huo alikuwa mdogo nami pia nilikuwa mdogo, lakini kwa kweli tulipendana sana mpaka tukaamua kuwaeleza wazazi nia yetu ya kuoana,” anasimulia mzee huyo.

Anasema yeye alikuwa mtoto pekee wa kiume kwa wazazi wake, baada ya kuhitimu elimu ya msingi, baba yake alimzuia kuendelea na masomo na badala yake alimtaka aoe, akihofia endapo angeenda shule, angeweza kukumbana na matatizo na kumpoteza.

“Nilioa nikiwa na umri mdogo kwa sababu baba alikataa nisiendelee na shule. Alisema siwezi kwenda mbali kwa sababu hana mtoto mwingine wa kiume.

“Nilipojaribu kutoka kwenda shule, walitumwa vijana kunifuata na kunirudisha. Nilirudi nyumbani na kufikiri kwamba nikishawaletea huyo mwanamke nitaendelea na shule, lakini sikupata tena nafasi hiyo wakati huo,” anasimulia.

Akiwa baba wa watoto 10, mzee Joseph amesema baada ya kuoa, aliendelea na maisha kwa kufuata misingi ya baba yake, hali iliyoimarisha ndoa yake na kuwawezesha kuishi maisha ya upendo, amani na kumcha Mungu siku zote.

Anasema baada ya kufunga ndoa na mkewe, licha ya kuishi kwao, baba yake aliendelea kumuusia kuishi maisha ya furaha, upendo na amani na mkewe.

“Hata tulipopata watoto wetu hawa, kila nilipokutana naye, aliendelea kutoa wosia kwangu kwamba niwalee wajukuu zake vizuri, wamche Mungu na wapendane,” anasema.

Anasema siri ya ndoa yao kudumu mpaka sasa wanasherehekea Jubilee ya miaka 75 ni kutokana na upendo, kumcha Mungu na kuvumilia na kuchukuliana kwa upole.

Ernest Joseph, mtoto wa kwanza wa mzee Joseph, anasema wamelelewa katika misingi ya upendo, kujituma na kufanya kazi kwa bidii.

“Tulichofundishwa ni tabia nzuri. Zamani si kama sasa, huwezi kumkuta mtoto wa kike ukamweleza upuuzi. Tuliwajua wasichana tukiwa wakubwa na siku zote baba na mama walifundisha upendo, bidii na kujituma katika kazi,” anasema Ernest.

Anasema wazazi wao wanakula vyakula vya asili kama ndizi, nyama, maziwa na waliwaelekeza njia sahihi za maisha.

Nini kifanyike ndoa za leo zidumu?

Ernest anaeleza ndoa nyingi za miaka ya karibuni huvunjika mapema kutokana na misingi mibovu inayowekwa tangu utotoni.

“Misingi inaanzia nyumbani. Wazazi wanapaswa kukaa na watoto wao, kuwaelekeza vizuri na kuwajengea nidhamu na heshima,” anasema Ernest.

Aidha, anarejea maandiko ya Biblia akisema, “Hata Biblia imesema usimnyime mtoto mapigo, maana ukimuacha dunia itamuangamiza.”

John Joseph, nduguye Ernest, anasema wazazi wao wamekuwa na nidhamu ya hali ya juu na wamewalea kwa misingi ya haki na bidii.

“Baba amekuwa mkali, lakini ni mtu wa haki. Anachukia uvivu na anasisitiza nidhamu ya kazi na kujitegemea,” anasema John.

Kwa upande wake, Padri John anasema ndoa ni safari inayohitaji maandalizi ya kina.

“Ndoa haianzi siku ya harusi, inaanza na maandalizi, lazima ujitambue na utambue unamchagua nani. Ndoa si chakula, si mapenzi ya mwili wala utajiri; ni uvumilivu, furaha na kuchukuliana,” anasema Padri John na kuongeza kuwa furaha katika ndoa hutegemea juhudi za pande zote mbili.

“Furaha haiwezi kupatikana nje ya umoja wa ndoa. Inahitaji kuchukuliana, kuvumiliana na kusameheana,” anasema.

Aidha, anatoa angalizo kwa vijana kuwa waangalifu katika kuchagua wenzi wao.

“Msichana au mvulana hujiunga nawe si kwa sababu ya kukosa kwao, bali kwa lengo la kujenga umoja. Umoja haujengwi kwa vitu, bali kwa moyo wa kushirikiana na kuelewana,” anasema.

Anawataka vijana kuacha mihemko na kuzingatia misingi ya upendo wa dhati, uvumilivu na kuheshimiana ili kujenga ndoa imara na ya kudumu.

Related Posts