Okrah amzuia beki mpya Yanga

MASHABIKI wa Yanga wanamuona beki mpya aliyetua hivi karibuni kutoka Singida Black Stars, Israel Mwenda mazoezini tu, lakini bado hajaweza kuruhusiwa kuanza kucheza lakini imefahamika kwamba tatizo ni winga wa zamani wa timu aliyewahi kupita pia Simba, Augustine Okrah.

Mwenda, ametua Yanga kwa mkopo kupitia dirisha dogo la usajili lililo wazi, lakini bado hajaanza kuichezea timu hiyo akiishia mazoezini tu huku kwenye mechi akiishia jukwaani tu, lakini nusanusa za Mwanaspoti zimejua chanzo cha beki huyo wa kulia kuishia kuwa mchezaji mtazamaji.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni kwamba Yanga haiwezi kumtumia Mwenda hadi pale itakapomalizana na Okrah, aliyeishtaki klabu hiyo Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kufuatia kuvunjiwa mkataba aliokuwa nao.

Bosi huyo wa TFF aliongeza kuwa, Okrah anaidai Yanga malimbikizo ya ada ya usajili ambayo hakumaliziwa hadi alipositishiwa mkataba mwishoni mwa msimu uliopita akiitumikia kwa muda wa miezi sita.

Hata hivyo, bosi huyo akaongeza kuwa, uongozi wa Yanga unafanya juhudi za kuindoa kesi hiyo ili klabu yao iweze kuendelea na matumizi ya Mwenda na mastaa wengine ambao watasajiliwa.

“Mwenda hataweza kucheza, waulizeni Yanga watawaambia lakini ishu ni Okrah aliwashtaki na wanatakiwa kumlipa, wakimalizana naye ndio hawa wapya mtaweza kuwaona,” alisema bosi huyo na kuongeza;

“Kuna juhudi zinafanywa na uongozi wa Yanga kumalizana na Okrah tunaziona lakini bila kufanya hivyo itakuwa ngumu kuwaona hao wachezaji wapya wakicheza. Huyu Mwenda hana tatizo kabisa usajili wake uko sawa lakini kesi ya Okrah ikimalizika ndio ataweza kuanza kutumika kucheza Yanga.”

Yanga ilimsajili Okrah katika dirisha dogo la msimu uliopita akitokea Becham United ya Ghana, lakini ikamuacha mara msimu ulipomalizika akiifungia bao 1 tu.

Related Posts