MSHAMBULIAJI wa Henan Jianye ya China, Opah Clement amesema chakula ni kati ya vitu vilivyompa changamoto nchini humo.
Nyota huyo alijiunga na timu hiyo akitokea Besiktas iliyokuwa inashiriki Ligi ya Uturuki ambako alimaliza na mabao nane.
Opah alisema kutokana na historia ya nchi hiyo kwenye milo ilimpa wakati mgumu wa kuchagua chakula hasa nyama akihofia huenda akakutana na mambo mengine.
“Nilipata tabu msimu huu, China wanakula vyakula vyao ambavyo Afrika kushika kazi sana, nilikuwa naangalia chakula hiki nakiweza nakula vingine naachana navyo unaweza kula unajua samaki kumbe mambo mengine,” alisema Opah.
Henan Jianye imemaliza ligi ikiwa nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi (11) ikisubiri kucheza mchujo wa Play-Off ili kujua kama itaendelea kusalia ama kushuka daraja.