KOCHA Msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma amesema timu yao imetumika kwa asilimia 70 mzunguko wa kwanza hivyo bado wana mikakati imara mzunguko wa pili ili kufikia malengo ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.
Singida Black Stars ipo nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 16 ikifanikiwa kukusanya poiti 33, imeshinda mechi 10, sare tatu na vipigo vitatu ikifunga mabao 22 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 11.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema malengo kwenye mzunguko wa kwanza wameyafikia kwa asilimia 70, bado wana kazi kubwa ya kufanya mzunguko wa pili kukamilisha ubora kwa wachezaji asilimia 30 zilizobaki ili kufikia malengo.
“Tumeona ubora na mapungufu yaliyopo kikosini baada ya mzunguko wa kwanza tukiwa nafasi ya nne kwenye msimamon tutarudi imara zaidi mzunguko huu wa pili ili kufikia mipango yetu ya kuipeleka Black Stars kimataifa,” alisema na kuongeza.
“Tunatambua mzunguko wa pili hautokuwa rahisi, ni jukumu letu sasa kuhakikisha tunairudisha timu ikiwa timamu na ipo kwenye ubora wa kutoa ushindani kwa wapinzani wetu.”
Akizungumzia kurudi kwa baadhi ya wachezaji ambao walitolewa kwa mkopo, alisema: “Ni kweli kuna wachezaji wamerudishwa na tayari wameanza maandalizi pamoja na timu ambayo sasa ipo mapumziko kwa wiki moja kuanzia Desemba 29, wakirudi tutaendelea na maandalizi.”
Wachezaji ambao walikuwa nje kwa mkopo na wamerudi Singida Black Stars ni kiungo Morice Chukwu aliyekuwa Fountain Gate, beki Hernest Malonga (Coastal Union) na kipa Fikirini Bakari (Fountain Gate).