Shinyanga. Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa zawadi ya chakula na vinywaji kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika kituo cha Buhangija kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Akikabidhi zawadi hizo jana, Desemba 29, 2024, kwa niaba ya Rais Samia, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amewasihi watoto hao kusoma kwa juhudi ili kufikia ndoto zao, huku akitumia fursa hiyo kuiasa jamii kuachana na imani potofu.
“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi hii kwa watoto hawa wenye mahitaji maalumu hapa Buhangija ili wafurahie na kusherehekea sikukuu ya mwisho wa mwaka. Nitumie fursa hii kuwaasa muendelee kusoma kwa bidii ili mtimize ndoto zenu. Msijione wanyonge, Serikali ipo pamoja nanyi kuhakikisha inawatengenezea mazingira rafiki ili mufikie ndoto zenu,” amesema Mtatiro.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Charles Luchagula, amesema zawadi zilizokabidhiwa ni mbuzi mmoja, mchele kilo 100, unga wa ngano kilo 50, unga wa semba kilo 50, sukari kilo 100, na mafuta ya kupikia lita 20.
Zawadi nyingine ni juisi katoni 50 na taulo za kike boksi mbili, vitu vyote vina thamani ya Sh1,480,000.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jumuishi Buhangija, Fatuma Jilala, amesema kituo hicho kina wanafunzi 146, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiunga mkono shule hiyo kwa kukamilisha ujenzi wa mabweni na kutatua changamoto mbalimbali.
“Wanafunzi watano wana ulemavu wa viungo, wasioona 27, viziwi 69, wenye ualbino 44 na uoni hafifu mmoja. Pia Serikali ilitupatia Sh190 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili na Sh16 milioni hutolewa kila mwezi kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu,” amesema Jilala ambaye pia ni mlezi wa kituo hicho.
Mmoja wa watoto hao, Elizabeth Emmanuel amemshukuru Rais Samia kwa zawadi hizo kwa ajili ya kufurahia sikukuu ya mwaka mpya.
“Naishukuru Serikali kwa kutambua uwepo wetu na kutuletea chakula na vinywaji ili nasi tufurahie na kusheherekea sikukuu. Hii inatupa faraja na kutokujihisi upweke,” amesema Elizabeth.