Samia, viongozi duniani waelezea upekee wa Rais Carter

Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa mataifa mbalimbali wamuelezea Rais wa 39 wa Marekani, Jimmy Carter, kuwa kiongozi mtetezi wa watu hasa waliopo mazingira hatarishi.

Carter amefariki dunia jana, Desemba 29, 2024 akiwa na miaka 100 chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya, Shirika la Habari Aljazeera limeeleza.

Kutokana na kifo cha Carter, Rais Samia ameungana na viongozi mbalimbali duniani kutuma salamu za pole kwa Serikali ya Marekani pamoja na familia ya kiongozi huyo.

Katika taarifa yake aliyoichapisha kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa X, Rais Samia ameandika,”Kwa niaba ya Serikali na watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natoa pole za dhati kwa familia ya Rais Jimmy Carter, Serikali na wananchi wa Marekani kufuatia kifo cha Rais mstaafu Jimmy Carter.

“Maisha ya Rais Carter katika utumishi wa umma yaligusa mamilioni ya maisha watu duniani kote. Atakumbukwa kama mfano kwa wale wanaotamani kutumikia jamii, mataifa yao na dunia kwa upendo na unyenyekevu.”

Pia Shirika la Aljazeera limenukuu salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi mbalimbali kutokana na kifo cha kiongozi huyo ambaye pia mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema Carter alikuwa mstari wa mbele kupigania amani mtetezi thabiti wa haki kwa makundi yaliyotelekezwa.

Naye Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, amesema Marekani imempoteza mtu aliyejitolea kupigania demokrasia.

“Dunia imepoteza mshauri mkuu wa amani, hasa kwa mashariki ya kati na mpigani haki,” amesema.

Kiongozi mwingine ni Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau aliyesema Carter ameacha alama kwenye uongozi wake, kwani alikuwa mtu mnyenyekevu, mwenye huruma na mchapakazi.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer amesema aliutambulisha uongozi wake kwa namna alivyojali haki za watu ndani na nje ya Taifa lake.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema moyo wa kiongozi huyo ulikuwa imara katika kupigania uhuru.

Kiongozi mwingine aliyetuma salamu za rambirambi ni Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, akimpongeza Carter kwa kazi yake ya kusimamia makubaliano ya amani ya mwaka 1978 kati ya Misri na Israeli – yanayojulikana kama mkataba wa Camp David – akisema utabaki katika historia.

Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, amemuelezea Carter kama kiongozi mpenda demokrasia na mtetezi wa amani.

Amesema Rais Carter alimshinikiza aliyekuwa dikteta wa Brazili kuwaachilia wafungwa wa kisiasa na kumkosoa kwa matumizi ya nguvu wakati wa utawala wake.

Nchini Panama ambako Rais Carter aliingia makubaliano mwaka 1977 ya kurudisha Canal ambayo wakati huo ilikuwa chini ya Marekani Rais Jose Mulino, amesema Carter alikuwa kiongozi mpenda demokrasia na aliisaidia Panama kupata uhuru wake kamili.

Vilevie, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema uongozi wa Carter “ulichangia kwa kiasi kikubwa amani na usalama wa kimataifa.”

Carter alikuwa Rais wa Marekani kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1981 akijizolea sifa ya kuwa msuluhishi wa migogoro duniani, jambo lililomfanya atunukiwe Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2002.

Pia Carter aliwahi kuandika historia ya kupanda Mlima Kilimanjaro mwaka 1988 na kwa mujibu wa tovuti ya Los Angeles Times, mwaka huo alifanikiwa kufika katika kilele cha Gilman.

Historia inaonyesha kuwa Carter aliyekuwa kada wa chama cha Democrats, ndiye Rais pekee wa Marekani aliyevunja rekodi ya kuishi umri mrefu.

Related Posts