Dar es Salaam. Kati ya mavuno na anguko, ni neno lipi linaakisi matokeo ya malengo uliyojiwekea kuyatimiza kabla ya kukamilika mwaka 2024? Kwa matokeo hayo, unajitathmini na kujiona wapi katika mwaka 2025?
Kama umevuna, hongera. Kwa walioanguka au kubaki kama walivyokuwa, ipo siri iliyojificha nyuma ya mafanikio ya kiuchumi na maendeleo kama inavyofafanuliwa na wanazuoni wa uchumi.
Hatua ya wanazuoni kutoa siri hiyo inakuja katika kipindi ambacho baadhi ya wananchi wameonyesha kutoshuhudia mabadiliko yoyote katika maendeleo yao binafsi mwaka 2024.
Miongoni mwa wananchi hao ni Abdallah Mpache, anayeishi jijini Dar es Salaam anayesema, hakuwa ameweka malengo, lakini alidhamiria kuwa 2024 ungekuwa mwaka utakaobadilisha maisha yake.
Hata hivyo, anasema anachokishuhudia ni tofauti na alivyotarajia, amebaki na hali ileile kama ilivyokuwa mwaka 2023, huku umri ukiendelea kusogea.
“Sina mabadiliko yoyote kiuchumi, nimebadilika mwili na umri, ngoja tuone 2025 itakuwaje,” anasema.
Neema Nicholaus, anayeishi pia Dar es Salaam, ana hadithi sawa na ya Mpache. Kwake uchumi unatokana na namna mwaka ulivyokuja.
“Kuna mwaka unakuwa wa kupata riziki, lakini 2024 hapana. Niliweka lengo la kupanga kwenye nyumba ya vyumba viwili nimeshindwa, bado nipo kwenye chumba kimoja,” anasema.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa wawili hao, Edgar Ngasongo ana simulizi tofauti, akisema kila alichokipanga kimekuwa katika mwaka 2024.
“Nilipanga ninunue kiwanja kabla ya kufikisha miaka 30, nimefanikiwa mwaka 2024 nikiwa na miaka 29, nilipanga nianze biashara nimefanikiwa, nilipanga nipate mtoto nimefanikiwa,” anasema.
Kama mwaka 2024 hukufanya lolote, anguko lako lilichochewa na kasoro na makosa binafsi uliyoyafanya katika mwaka husika, kama inavyoelezwa na mwanazuoni wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benedict Mongula.
Siri ya kuibadili hali hiyo iwe mafanikio, anasema ni kuyatambua makosa yako na kujisahihisha kwa kuhakikisha unaenenda inavyopaswa.
“Kama ulikuwa mlevi na unaona ndiyo tabia iliyokwaza mafanikio yako, jisahihishe kwa ama kuacha au kupunguza. Kama ulikuwa na tabia yoyote iliyokuangusha, iache ili uinuke,” anasema.
Pamoja na umuhimu wa hatua binafsi, mwanazuoni huyo anaona kuna mambo huwa nje ya uwezo wa mtu kuyabadilisha au kuyafanya yatokee.
Kwa mujibu wa Profesa Mongula, miongoni mwa mambo hayo ni yale yanayohitaji uwezo wa kipato ili kuyafanikisha, ikiwemo kuanzisha au kukuza biashara.
Katika hayo, anaeleza ni muhimu Serikali na mashirika ya uwezeshaji, yatimize wajibu wa kuhakikisha yanawezesha ili watu wainuke kiuchumi na kupata maendeleo.
Kuhusu malengo, mwanazuoni huyo anasema ni muhimu wakati unayaweka, utafakari pia na namna ya kuyatimiza, ili yasibaki kuwa mipango kwenye karatasi.
“Tafakari kama unataka kufanikiwa, unapaswa kujua vitu vyote vinavyohitajika ili kutimiza malengo husika,” anasema.
Kutojitambua, kutotafuta na kutumia fursa kulingana na mazingira uliyopo na kukosa nidhamu ya fedha, ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa na Profesa Mongula, kukwamisha safari ya maendeleo ya wengi.
“Watu wanachukulia maisha ni kitu rahisi, wanajiendea kusubiri bahati wakati maisha si bahati na wengine wanajikatia tamaa,” anasema.
Kutokana na uhalisia huo, anasema Serikali ina kazi ya kufanya kuhakikisha inawaamsha vijana, kuwapa matumaini, kuwaonyesha na kuwapa fursa.
Mhadhiri mwingine wa uchumi wa UDSM, Dk Hamisi Mwinyimvua anasema malengo yanayowekwa yanapaswa kuakisi uwezo wa mtekelezaji.
“Malengo yanapaswa yaendane na nyenzo, yanaweza kuwa malengo mazuri, lakini jinsi ya kufanya ndicho kinachowakwamisha wengi,” anasema.
Dk Mwinyimvua anasema malengo yanakuwa hai kwa wale wenye uhakika wa kipato cha kutekelezea lengo husika.
Mwanazuoni huyo anasisitiza, baadhi ya watu wanajiwekea malengo makubwa bila kupima uwezo na jinsi ya kuyatekeleza, hivyo yanabaki hewa.
“Hii ni kama bajeti, unaweza kutengeneza kubwa lakini kama hujui utatoa wapi fedha za kutekelezea bajeti husika hutafanikiwa.
“Muhimu ni kuwa na malengo yanayoendana na uwezo wa utekelezaji wake,” anasisitiza Dk Mwinyimvua.
Mtazamo kama huo umetolewa pia na mwanazuoni mwingine wa uchumi, Julieth Tibanywana anayesema makosa yanayofanywa na wengi, ni kuweka malengo bila kujua namna ya kuyatimiza.
“Unapoweka malengo unatakiwa kuwa na kazi unayofanya au biashara itakayokupatia fedha itayowezesha kutimizia malengo husika,” anaeleza.
Anasema ni kosa katika mafanikio kuweka lengo kinyume na uhalisia wa kipato halisi, maana itashindikana kulitekeleza.
“Ni vema kuoanisha malengo na shughuli au kipato chako,” anasisitiza.
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917