TGNP Yaleta Pamoja Jamii Kujadili Malezi Bora na Ulinzi wa Watoto

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), umewakutanisha wazazi, walimu na wanafunzi kutoka vilabu vya jinsia kwaajili ya kushirikishana mafanikio kupitia vilabu hivyo shuleni.

Akizungumza wakati wa mdahalo huo uliofanyika leo Desemba 30,2024 katika viwanja vya TGNP- Mtandao Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi amewataka wazazi pamoja na walimu kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha wanawasaidia watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Amesema wamekuwa wakikutana na wazazi na walimu na kuwaambia ni mazingira gani salama yatengenezwe kwaajili ya watoto wetu kuepuka na vitendo vya ukatili kwenye jamii inayowazunguka.

“Kipindi ambacho tumekutana na wazazi, walimu na watendaji wa serikali za mitaa, tulizungumza kwamba kauli chanya kwa watoto ni muhimu sana, tumezoea watoto wetu kuwapa kauli hasi ambazo zinamfanya kuwa na uhasi. Badala umwambie mtoto unasoma vizuri ukiw amkubwa utakuwa kiongozi fulani, mtoto anakuwa anaelewa kumbe nikisoma vizuri nakuwa mtu fulani”. Amesema Liundi.

Aidha Liundi amewataka wazazi kuhakikisha wanatambua vipaji vya watoto wao na kuviendeleza kwani sekta ya sanaa kwasasa imekua na inatoa ajira nyingi.

Kwa upande wake Flora Ndaba kutoka Idara ya Ujenzi wa nguvu za pamoja na harakati TGNP, amesema wamewakutanisha vilabu vyote vya jinsia vilivyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo mwakani wanatarajia kushirikisha na vilabu vilivyopo katika nchi nzima ili kujadili kwa pamoja na kutatua changamoto za watoto.

Amesema watoto waliopo kwenye klabu za jinsia walikuwa sehemu ya kushirikishwa katika kutoa maoni yao namna ya utekelezaji wa Dira ya 2025 na namna gani Dira ya 2050 iandikwe ikiakisi matamanio ya watoto tukikua kwamba miaka 25 ijayo hawa watoto watakuwa viongozi kwenye nchi yetu na kutuletea maendeleo.

Kwa upande wake Mwalimu kutoka shule ya Sekondari Kerezange, Madamu Halima Msangi amesema vilabu vya jinsia shuleni vinawasaidia walimu kuimarika namna ya kuwapa wanafunzi malezi yaliyokuwa bora kwa kusikiliza maoni yao na kueleza changamoto zinazowakabili.

“Suala la malezi mwalimu anasimama kwa asilimia 100, mzazi anakuwa hasa kwenye masuala ya makuzi kwa watoto, ninajitahidi kuwapa watoto malezi yaliyobora na ambayo yatakuwa na manufaa kesho”. Amesema Madamu Halima.

Pamoja na hayo Madamu Halima ameiomba Serikali kuandaa midahalo ambayo itawakutanisha walimu na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanajihusisha na suala la malezi na jinsia ili kuwasaidia vijana wetu ambao wapo katika makuzi.

Hata hivyo kwa upande wa Wazazi, Gidioni Muna ameipongeza TGNP kwa kuweza kuwakutanisha na kujadili pamoja kuhusu malezi na makuzi kwa watoto, hivyo amewaomba kuongeza ushiriki kwa walimu na walezi wengi.

Nao wanafunzi wamepongeza uwepo wa klabu za jinsia mashuleni kwani inawapa ujasiri wa kusema changamoto ambazo wanakutana nazo hasa vitendo vya ukatili.




























Related Posts