TTB Yawahimiza Wananchi Kutembelea Vivutio vya Utalii Msimu wa Sikukuu

Na Mwandishi wetu Dodoma

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imewahimiza wananchi kutumia msimu wa sikukuu na likizo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kujifunza, kuburudika, na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Ernest Mwamwaja, alisema Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vya kipekee ambavyo vinapaswa kuthaminiwa na Watanzania wenyewe.

“Msimu huu wa sikukuu ni fursa muhimu kwa wananchi kutembelea vivutio vilivyopo nchini ili kujivunia urithi wetu wa asili na kiutamaduni,” alisema Mwamwaja.

Aliongeza kuwa, “Tulizindua kampeni maalumu ya kuhamasisha utalii wa ndani katika msimu huu wa sikukuu ijulikanayo kama ‘Funga Mwaka Kijanja Talii,’ inayolenga kuwahamasisha Watanzania wa rika zote kushiriki katika shughuli za utalii. Kampeni hii itakoma ifikapo Januari 10, 2024.”

Mwamwaja alisema TTB imejipanga kushirikiana na waandishi wa habari ili kuongeza idadi ya watalii, kwa lengo la kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 inayolenga kufikia watalii milioni tano.

Aidha, alisema jitihada hizo pia zinaunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kukuza sekta ya utalii na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Tunaamini kupitia waandishi wa habari tunaweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na kutangaza vivutio vya utalii, ili kuongeza idadi ya watu wanaotembelea vivutio vyetu,” alisema Mwamwaja.

Alisisitiza kuwa ni muhimu wananchi kuchangamkia fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Nchini



Related Posts