Ufaulu darasa la Saba Zanzibar wapaa, 642 wakizuiliwa matokeo kwa udanganyifu

Unguja. Baraza la Mitihani Zanzibar, limetangaza matokeo ya darasa la saba yanayoonyesha ufaulu kupanda kwa asilimia 1.66 kutoka asilimia 95 ya mwaka jana hadi kufikia asilimia 96.66, huku watahiniwa 642 matokeo yao yakizuiliwa kwa udanganyifu.

Akitangaza matokeo hayo leo Jumatatu, Desemba 30, 2024 katika Ofisi za Wizara ya Elimu, Mkurugnzi Mtendaji wa baraza hilo, Dk Rashid Abdulaziz Mukki, amesema watahiniwa 44,486 waliofanya mitihani huo wamefaulu kwa madaraja ya A, B, C na D huku watahiniwa 1,535 sawa na asilimia 3.34 wakipata daraja F.

“Kati ya watahiniwa waliofaulu, wanaume ni 20,571 sawa na asilimia 46.24 na wanawake 23,915 sawa na silimia 53.76. Ufaulu wa mwaka 2024 umeongezeka katika madaraja ya C na D, huku watahiniwa waliopata daraja la F wamepungua kwa asilimia 1.66 kutoka asilimia 5.00 mwaka 2023 hadi asilimia 3.34,” amesma

Amesema ufaulu wa masomo kwa ujumla kwa mwaka 2024 unaonyesha somo la Creative Arts and Sports na Social Science ndio yenye ufaulu wa juu wa zaidi ya asilimia 99.68,  ikilinganishwa na mwaka 2023, yalikuwa na ufaulu wa asilimia 99.86.

Pia, somo la lugha ya Kiswahili ufaulu umependa kwa asilimia 94.87, ikilinganishwa na asilimia 89.32 mwaka 2023. Somo la Hisabati ufaulu wake umepanda kwa asilimia 55.52, ikilinganishwa na sailimia 50.10.

Wakati ufaulu ukiongezeka, baraza limesema kumebainika viashiria vya udanganyifu kwa watahiniwa 642 kutoka vituo 25 ambao matokeo yao yamezuiliwa.

“Wasimamizi wa mitihani na wale wote watakaobainika na makosa ya kujihusisha na udanganyifu wa mitihani watachukuliwa hatua za kinidhamu,” amesema Dk Rashid.

Kadhalika, uongozi wa shule zitakazobainika kufanya udanganyifu katika uwasilishaji wa alama endelevu kwa mtihani huo, nao watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Kwa mujibu wa taarifa ya baraza hilo, watahiniwa 927 waliosajiliwa hawakufanya mtihani. Hata hivyo, idadi hiyo inatajwa kupungua, ikilinganishwa na watahiniwa 1,152 ambao hawakufanya mtihani mwaka 2023, sawa na silimia 19.53.

Wakizungumzia matokeo hayo, baadhi ya wadau wa elimu akiwemo Dalhat Hussein, amesema ufaulu ni jambo moja, lakini ubora wa elimu ni jambo lingine.

“Tunaposhangilia ufaulu kuongezeka tuangalie pia aina yetu ya elimu kama ni shindani, ikilinganishwa na teknolojia ya sasa ya mabadiliko ya dunia,”amesema.

Related Posts