Wanaodaiwa kuiba shehena ya petroli, dizeli wataka upelelezi uharakishwe

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa saba katika kesi ya wizi wa shehena ya mafuta ya petroli na dizeli yenye jumla ya lita milioni 9.9, Gaudence Shayo ameomba upande wa mashtaka uharakishe upelelezi ili wajue hatima yao.

Shayo ametoa maelezo hayo leo Jumatatu, Desemba 30, 2024, baada ya wakili wa Serikali, Titus Aaron, kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa shauri hilo unaendelea, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

“Mheshimiwa hakimu, tunaomba hawa upande wa mashtaka wakamilishe haraka upelelezi wa kesi yetu ili tudhaminiwe,” ameeleza Shayo.

Akijibu ombi hilo, wakili Aaron amedai kesi inayowakabili washtakiwa hao haina dhamana, kwa kuwa miongoni mwa mashtaka yanayowakabili lipo la kutakatisha fedha.

Kuhusu upelelezi, Aaron amedai atafuatilia kujua umefikia hatua gani.

Baada ya kusikiliza maelezo ya wakili na mshtakiwa huyo, Hakimu Nyaki ameahirisha kesi hadi Januari 15, 2025 itakapotajwa.

Shayo na wenzake saba wanakabiliwa na mashtaka 20, yakiwemo ya kutakatisha fedha na wizi wa mafuta ya petroli na dizeli na kuisababishia hasara kampuni ya kimataifa ya kuhifadhi mafuta (Tiper) Tanzania ya zaidi ya Sh26 bilioni.

Mbali na Shayo, washtakiwa wengine ni Tino  Ndekela ambaye ni  dereva wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mfanyabiashara Fikiri Kidevu, Amani Yamba, Mselem Abdallah, Kika Sanguti, Twaha Salum na Hamisi Hamisi.

Related Posts