Wapiga makachu wapigwa msasa, kufunguliwa kesho

Unguja. Wakati mchezo wa makachu ukifunguliwa kesho Desemba 31, 2024 Jumuiya ya  Waratibu na Waendesha Misafara ya watalii Zanzibar (Zato), imewapa mafunzo maalumu vijana hao ili kuendana na matakwa na miongozo ya utalii.

Mwenyekiti wa Zato, Khalifa Mohamed Makame amesema wamefikia hatua hiyo baada ya bodi ya Zato kuona kuna haja ya kuwapa elimu vijana hao, kwani wamekuwa sehemu ya bidhaa za utalii.

“Sisi makachu tunaichukulia kama bidhaa ya ziada iliyoongezeka katika huduma tunazozitoa kwenye utalii, hivyo inatakiwa ilindwe, ijengwe  ili iwe na mustakabali mwema kwa Wazanzibari,” amesema.

Amesema ndani ya kipindi kifupi yametokea matukio matano kwa wakati mmoja mambo ambayo yakiachwa yaendelee yanaweza kuleta tatizo.

Amesema wamebaini kinachokosekana kwa vijana hao ni weledi wanapofanya shughuli hizo na msaada wa kuwa na wanachama waadilifu na waaminifu wenye maadili.

“Kwa hiyo tunapowaangalia hawa vijana tunajiangalia kama sisi, tukiona wanachopitia tunawajibika kutia uso tuwasaidie hata katika kuchagua mtu sahihi katika uongozi wetu.”

Baadhi ya vijana hao wamekiri kuna baadhi ya matukio ambayo yalitokea kwa sababu ya kukosekana weledi wa kitaaluma.

Rais wa makachu, Hanafiy Said Salim amesema wamejifunza kutokana na makosa lakini watazingatia mafunzo waliyopewa yakiwamo ya kuzingatia maadili.

Naye kiongozi wa nidhamu wa kundi hilo, Omar Bakar Khalfan amesema, “tunakutana pale kila mmoja na tabia zake, jamii isituchukulie kama ni watu wasiokuwa na uadilifu isipokuwa ni watu wachache wanaotaka kuharibu taswira ya mchezo huo.

Katibu wa kundi hilo, Ali Saleh amesema “tunaweza kusema tunashukuru kutokana na kosa lile kwani kuna mambo mengi tulikuwa hatuyajui, lakini baada ya tukio hili tumefahamu na tumepewa mafunzo, hivyo lazima tusijisahau kufanya vitu visivyofaa,” amesema.

Mamlaka ya Uhifadhi na Uendeshaji Mji Mkongwe ilisitisha kwa muda mchezo wa makachu Forodhani tangu Desemba 22, 2024 baada ya kusambaa picha mjongeo iliyoonyesha mwanamke akiruka akiwa amevalia nguo ambazo ni kinyume na maadili ya utamaduni wa Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na kuthibitishwa na mkurugenzi wa Mji Mkongwe, Ali Abubakar, ilieleza wamechukua hatua hiyo kutokana na matukio ya ukiukwaji wa sheria na miongozo.

Akielezea wanapofunguliwa kesho nini kifanyike, Ali amesema watakaoruhusiwa ni wale watakaokubaliana na miongozo iliyowekwa kwa kufuata misingi ya maadili

Matukio hayo ni pamoja na upigaji makachu kwa kutumia mavazi yanayokwenda kinyume na utamaduni, uharibifu mkubwa wa mifereji na miundombinu mingine pamoja na matumizi ya debe za taka kwa michezo ya vichekesho.

Related Posts