MABOSI wa ‘Chama la Wana’, Stand United wameanza kuboresha kikosi hicho katika dirisha hili dogo kwa kuingiza nyota wapya watano watakaoongeza morali na wale waliopo, kwa lengo la kuhakikisha timu hiyo inapanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
Timu hiyo yenye maskani mjini Shinyanga, imenasa saini ya aliyekuwa nyota wa Mtibwa Sugar, Yanga, Simba, Ndanda na Pan Africans, Kigi Makasi na washambuliaji, Lucas Sendama aliyetokea Biashara United na Aniceth Revocatus kutoka Pamba.
Wengine ni kiungo, Khalid Kibailo aliyetokea Copco FC ya jijini Mwanza na winga, Seleman Richard, ikiwa ni usajili ambao umepokewa kwa shangwe na kocha mkuu wa timu hiyo, Feisal Hau anayeamini utaleta mabadiliko chanya katika kikosi hicho.
“Nashukuru viongozi wamefanya kazi yao vizuri kwa kuongeza wengine wapya kwa sababu tangu msimu huu umeanza tulikuwa na kikosi kidogo na kusababisha wengi wao kutopata muda wa kupumzika, mwelekeo kwa sasa ni mzuri kikosini,” alisema Feisal.
Feisal aliyekuwa Kocha wa Copco FC, amechukua nafasi ya Meja Mstaafu, Abdul Mingange aliyejiunga na Songea United, huku akipambana kuirejesha Stand United Ligi Kuu, baada ya kushuka msimu wa 2018-2019, ilipomaliza nafasi ya 19 kwa pointi 44.