Baada ya shamrashamra za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, wazazi wengi wamejikuta wakikumbana na hali ngumu ya kifedha.
Kwa walio wengi, Januari ni mwezi wenye vilio, na mikasa ya kudaiana kwa familia nyingi. Wakati watoto wakitarajiwa kurudi shuleni, wazazi hukosa fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya watoto wao.
Katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, na Arusha, hali huwa ni mbaya zaidi, huku baadhi ya familia zikiingia katika madeni au kutumia mikopo ya Vikoba ili kuhakikisha watoto wao wanarejea shuleni kwa wakati.
Ni wazi kwamba wazazi wengi walijizatiti kugharamia likizo na sherehe za mwaka mpya, lakini wakati huu wa kulipa ada za shule huwa ni mtihani mkubwa.
Wakati baadhi ya wazazi wanazungumzia ugumu wa kumudu gharama za shule, wengine wanachangia kwa makusudi hali hii kwa kupuuzia majukumu yanayowakabili siku za usoni, ambapo wengi hujiingiza katika sherehe za sikukuu kwa kufanya matumizi yasiyo na ulazima.
“Tunaishia kumalizia hadi senti ya mwisho kwa kusherehekea Krismasi kupita kiasi, na hatufikiri mbele kwa suala la watoto wetu kurudi shuleni,” anasema mmoja wa wazazi anayeishi jijini Dar es Salaam.
Ni kweli kwamba, sherehe za likizo, ununuzi wa mavazi mapya, na matukio ya kijamii hufanya wazazi wengi kupoteza mwelekeo wa kifedha kwa kipindi hicho, huku wakisahau kwamba Januari inakuja na hitaji la kuwalipa walimu na michango ya shule liko palepale.
Ingawa baadhi ya shule za umma zimeondoa ada za moja kwa moja kupitia sera ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, gharama nyingine, kama vile michango ya wazazi vifaa vya shule, usafiri, na ada za ziada, zimekuwa changamoto kubwa kwa familia maskini.
Hali hii imekua tishio kwa familia nyingi, na hasa kwa wale walioko katika maeneo ya vijijini na miji midogo ambapo hali ya kiuchumi si nzuri.
Mwalimu Lasuli Ikizu wa jijini Dar es Salaam anasema: “Mwaka huu hali imekuwa ngumu zaidi. Wazazi wanakimbizana kutafuta fedha za kulipa ada, na wengine hawawezi kumudu gharama hizi. ‘’
Anaongeza: ‘’Ni vigumu kwa wengi wetu. Hata walimu tunakutana na hali ya kutolipwa kwa wakati, hasa katika shule binafsi ambapo malipo ya ada yanacheleweshwa na hivyo kuathiri ustawi wa familia zetu.”
Mwalimu Ikizu anaelezea kwamba, licha ya shule kuwa na bajeti ya kulipa walimu, bado kuna changamoto kubwa ya kifedha, hasa wakati wa likizo.
“Inapofika Januari, tunakutana na changamoto kubwa. Wakati mwingine, hata kama shule ina bajeti ya kulipa walimu kwa mwaka mzima, malipo yetu yanacheleweshwa kutokana na sababu za kifedha, na hii inaathiri familia nyingi,” anasema.
Wakati shule nyingi zinakuwa na michango ya ziada, kama vile vifaa vya shule, karatasi, na michango ya ziara za kimasomo, wazazi wanajikuta wakichangia pesa nyingi zaidi ili watoto wafanikiwe kujiunga na masomo.
Hii ni changamoto kubwa kwa wazazi ambao tayari wanakabiliwa na upungufu wa fedha baada ya matumizi ya likizo.
Mwalimu Anjela Mwasu kutoka jijini Mwanza anaelezea hali hii kwa kusema: “Hali hii imekuwa ni kawaida. Wazazi wanapaswa kulipia vifaa vya shule, na wakati mwingine wanapaswa kulipia ziara za kimasomo ambazo zinakuwa na gharama kubwa. Hii ni changamoto kwa wazazi wengi, hasa wale wa familia masikini.”
Naye mwalimu Amani Ngowi kutoka Arusha, anasema: “Madhila haya hutokea kila mwaka, lakini mwaka huu ni mbaya zaidi. Tumekutana na familia nyingi ambazo zinahitaji mikopo ili watoto wao warudi shuleni. Hali hii ni ngumu kwa wazazi wengi, na inahitaji ufumbuzi wa haraka.’’
Mwalimu huyo anasema ingawa sera ya elimu bure, imeondoa ada, bado gharama nyingine zinaendelea kuwa kikwazo.
Utafiti wa kimataifa unaonyesha kuwa katika nchi nyingi, mzigo wa gharama za elimu unakuwa mkubwa kwa familia maskini, na hili linazuia watoto wengi kutimiza haki yao ya elimu.
Katika nchi kama Zambia na Tanzania, wazazi wengi wamejizatiti kutafuta njia za kulipia ada na gharama nyingine za elimu, lakini wengi wao wanajikuta wakishindwa kumudu.
Katika hali hii, wamiliki wa shule binafsi wanakubaliana kwamba, licha ya changamoto za kifedha, lazima ada ilipwe kwa wakati ili shule ziendelee kutoa huduma.
“Hatuwezi kutoa elimu bure, kila mwaka tunakutana na changamoto za kifedha. Wakati mwingine tunakosa fedha za kulipa walimu na kugharamia masuala mengine muhimu kama vile vifaa vya shule,” anasema Mwalimu Mwasu kutoka Mwanza.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wazazi waemekuwa wakitafuta njia bora za kugharamia elimu.
Mmoja wa wazazi jijini Dar es Salaam, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, anasema: “Hali ya fedha imekuwa ngumu kwa wazazi wengi. Tumekuwa tukitumia mikopo ya Vikoba ili kumudu gharama za shule. Ingawa watoto wetu wanapenda shule, ni vigumu kuwa na fedha za kutosha kulipia ada na gharama nyingine zinazohusiana na elimu.”
Hata hivyo, katikati ya lindi hili la changamoto za kifedha, wapo wazazi wanaowatoa watoto kutoka shule za umma ambazo ada ni bure kwenda shule binafsi.Hii wanasema inatokana na uhitaji wa elimu bora na huduma bora zinazotolewa katika taasisi binafsi.
Ingawa baadhi ya shule za serikali zinatoa elimu bure, wazazi wanatatizwa na ubora wa elimu na huduma zinazotolewa.
Mwalimu Ngowi anaeleza, “Wazazi wengi wanapeleka watoto wao shule binafsi kwa sababu wanapata huduma bora. Hata hivyo, hili ni suala la kiuchumi, kwani si kila mzazi anaweza kumudu gharama hizo.”
Hata hivyo, katika mazingira haya ya matabaka ya watoto wanaosoma shule bora na zile zinazojikongoja, wadau wanasema Taifa linaongeza pengo kati ya watoto wa familia maskini na watoto wa familia tajiri.
Ukata wa kifedha katika sekta ya elimu unahitaji mjadala wa kina, na hasa katika jamii maskini ambapo gharama za masomo zinakuwa kikwazo kikubwa kwa watoto wengi kutimiza ndoto zao.
Wazazi, walimu, na wamiliki wa shule binafsi wanapaswa kujitahidi kutafuta suluhisho bora ili watoto wote waweze kupata elimu bora bila kuathiriwa na hali ya kifedha.
Serikali inapaswa kuzingatia hii na kuimarisha sera za elimu ili kutoa fursa sawa kwa watoto wote, bila kujali hali zao za kifedha.