Benjamin Mkapa kuwekeza katika upasuaji wa Robot

Dodoma. Wakati zimebaki saa chache kumalizika kwa mwaka 2024, Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imetangaza mipango yake ya kuwekeza katika teknolojia ya upasuaji wa kutumia roboti (Robotic Surgery) ili kurahisisha kazi kwa wataalamu na kuboresha huduma za afya.

Akizungumza leo, Jumatano Desemba 31, 2024, jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi amesema hospitali hiyo imefanikiwa kufanya upandikizaji wa figo kwa mafanikio na mgonjwa wa 50 tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo Machi 22, 2018, amepata huduma hiyo.

Profesa Makubi amefafanua kuwa BMH ilikuwa kituo cha pili nchini kuanza kutoa huduma za upandikizaji figo.

“Kati ya wagonjwa hao, 50 waliopandikizwa figo, asilimia 95 wanaendelea na maisha ya kawaida. Katika mwaka 2025, hospitali inapanga kuongeza kasi ya huduma za upandikizaji figo kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwamo uvunaji wa figo kwa njia ya matundu madogo badala ya upasuaji wa sehemu kubwa ya mwili,” amesema profesa huyo.

Aidha, Profesa Makubi amesema BMH inatarajia kupanua kituo cha matibabu ya figo na kukifanya kuwa cha umahiri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa ufadhili wa Serikali ya Japan, kwa gharama ya takribani Sh33 bilioni. Pia, ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) utaimarishwa, hasa katika mafunzo ya Robotic Surgeries.

Kuhusu mgonjwa wa 50 aliyepandikizwa figo, Emmanuel Woiso (38), Profesa Makubi amesema ameruhusiwa kurejea nyumbani leo baada ya matibabu kufanikiwa.

Woiso ameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya nchini na kuwezesha huduma hizo kupatikana ndani ya nchi.

Profesa Makubi pia amezungumzia gharama za matibabu, akisema Serikali hutumia wastani wa Sh34 milioni kwa kila mgonjwa wa figo nchini, ikilinganishwa na wastani wa Sh64 milioni kwa matibabu nje ya nchi.

Kwa wagonjwa 50 waliotibiwa BMH, Serikali imeokoa takribani Sh1.6 bilioni.

Kwa upande wake, Emmanuel Woiso amesema awali alitembelea hospitali kadhaa kabla ya kushauriwa kufika BMH.

“Baada ya vipimo kufanyika na operesheni kufanikiwa, sasa najisikia na afya njema na ninaweza kuendelea na shughuli zangu za kila siku,” amesema.

Hata hivyo, Profesa Makubi ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya, hatua ambayo imewezesha huduma za kibingwa kupatikana nchini.

Related Posts