MFUKO wa Serikali ya Zanzibar umenufaika kwa kupata kiasi cha Sh. 3 bilioni zikiwa ni thamani ya mali mbalimbali zilizotaifishwa kwa kuhusishwa na biashara ya madawa ya kulevya. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Kamishna wa Mamlaka ya Kupambana na Madawa ya Kuelvya Zanzibar, Kanali Burhan Zubeir Nassor anasema mali zilizotaifishwa ni pamoja na nyumba, vyombo vya usafiri ikiwemo magari na Boti na fedha taslim.
Kanali Burhan amewaambia waandishi wa habari kuwa madawa ya kulevya yanaendelea kupenyezwa Zanzibar na milango mikuu ya kupitishia ni Bandari ya Majahazi Malindi na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume [AAKIA] uliopo Kisauni nje kidogo ya jiji la Zanibar.
Ameeleza hayo wakati akitangaza kukamatwa kwa madawa ya kiasi cha Kilogramu 798 kwa mwezi Novemba peke yake.
“Madawa haya yakitumika yanaweza kutengenezewa vidonge milioni 27 ambavyo vikigawiwa kwa wananchi wa Zanzibar kila mmoja atapata vidonge 14,” alisema.
Kanali Burhan alisema Mamlaka imeendelea kupata mafanikio makubwa ya kudhibiti biashara ya madawa ya kulevya tangu kufanyiwa marekebisho sheria ya kudhibiti iliyoanzisha mamlaka hiyo.
Marekebisho hayo ya mwaka jana 2024 yalihusu kuipa Mamlaka uwezo wa kukamata watuhumiwa, kuwachunguza na kuwashtaki mahakamani.
Ndio kusema Mamlaka hiyo sasa ina uwezo unaofanana na Jeshi la Polisi ambalo Kikatiba ndilo lenye jukumu la kukamata, kupeleleza na kufungulia mashtaka watuhumiwa kwa kuahirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar [DPP].
Ni Mamlaka hii ya kudhibiti Madawa ya kulevya sasa inatajwa askari wake kuhusika na tukio la kuuliwa kwa kipigo wakaazi watatu wa kijiji cha Kiungoni, Jimbo la Pandani, wilayani Wete, Kaskazini Pemba.
Katika tukio hilo, watu watatu walikamatwa kwa tuhuma za kumiliki madawa ya kulevya na wawili kati yao, Amour Khamis Salum mwenye umri wa miaka 28 na Othman Hamad Othman umri wa miaka 75 walirudishwa nyumbani wakiwa maiti na familia zao kulazimishwa kuwazika usiku.
Mwenzao Hamad Mbarouk alikutwa siku ya pili akiwa ametupwa msituni amefariki.
Wenyeji wanasema walikamatwa na askari wa kikosi cha Madawa ya Kulevya ambacho hutumia Polisi na askari wa vikosi vingine.
Walirudishwa kwa gari ya Kikosi cha Valantia lakini waliokabidhi miili na kusimamia uchimbaji wa makaburi walikuwa Jeshi la Kujenga Uchumi [JKU].
Katika hali ya kushtua, ripoti za daktari kuhusu miili hiyo zinaeleza kuwa mmoja alikufa kwa pumu wakati miili imejaa majeraha ya vipigo.