Dar es Salaam. Familia ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mstaafu, Jaji Frederick Werema imesema kifo chake kimeacha simanzi na pengo, likiwamo la ushauri.
Jaji Werema alifariki dunia jana Desemba 30, 2024 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 31, nyumbani kwa marehemu Mikocheni A, jijini Dar es Salaam, mdogo wa marehemu ambaye ni msemaji wa familia hiyo, Japhet Werema amesema:
“Alikuwa mtu ambaye hapendi kumpa mzigo wake mtu mwingine, kama anaona mzigo anastahili kuubeba basi anaubeba na si mtu mwingine lakini pia alikuwa na uwezo wa kuwabebea wengine mizigo yao.”
Amesema hata ndani ya familia alibeba mizigo mingi, akieleza hakuwa tayari kukubali au kuona mtu akisingiziwa uongo wakati anayetakiwa kuwajibika anajulikana.
“Hakuwa mtu anayependa kubebesha watu mizigo, amesaidia zaidi majirani hasa katika eneo la kusomesha watoto. Kifo chake ni pengo kubwa,” amesema.
Japhet amesema Jaji Werema alikuwa kaka yao mkubwa, akieleza baba yao alikuwa na watoto wengi si chini ya 20.
“Jaji Werema alikuwa mkubwa ingawa kuna wakubwa waliotangulia mbele ya haki. Yeye alikuwa mkubwa na tulikuwa tunamtegemea kama kiongozi,” amesema.
Japhet amesema: “Tulizipokea taarifa za kifo chake kwa masikitiko makubwa kwa kuwa ni mtu tumekaa naye kwa muda mrefu na alikuwa kaka na kiongozi wa familia yetu. Alikuwa mshauri na mwenye msaada.”
“Tukiwa na shida kwenye familia yeye alikuwa anachukua nafasi kubwa ya kutusaidia kwa yanayotukuta katika kupata suluhu, alikuwa kiongozi mzuri hasa kwa sisi wadogo zake,” amesema.
Japhet amesema siku ya jana Desemba 30, akiwa nyumbani kwake Jaji Werema alijihisi vibaya kiafya akamuomba mkewe ampeleke Hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi.
“Baada ya kufika Muhimbili alikaa kwa muda kidogo, hali yake ilibadilika ghafla na kufariki dunia. Hadi sasa hatujajua tatizo hasa lilikuwa nini na bahati isiyokuwa nzuri madaktari hatukuwauliza,” amesema.
Japhet amesema taarifa za kifo alizipata kutoka kwa shemeji yake ndipo alipokwenda Muhimbili.
Amesema Jaji Werema ameacha mjane, watoto watatu na wajukuu watatu.
“Ratiba ya mazishi yatafanyika Kijiji cha Mguto, kesho Januari Mosi, 2025 mwili tutautoa Hospitali ya Jeshi Lugalo na utaenda Kanisa Katoliki la St. Martha lilipo Mikocheni B kwa kuwa alikuwa muumini na mwenyekiti wa Parokia ya pale,” amesema.
Amesema baada ya ibada mwili utapelekwa nyumbani kwake na Januari 2, 2025 utapelekwa Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuagwa.
“Januari 3, 2025 mwili utapelekwa uwanja wa ndege kwa ajili ya kusafirishwa kwenda mkoani Mwanza na baadaye Butiama, mkoani Mara,” amesema.