Jamii yaaswa kusaidia watoto yatima

Dar es Salaam. Wito umetolewa kwa jamii kuwasadia watu wenye mahitaji maalumu ili nao washerehekee mwaka mpya kwa furaha.

Hayo yamelezwa leo Desemba 31, 2024 na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wajomba Family, Salum Ally wakati wa utoaji wa misaada kwa watoto yatima Wilaya ya Kigamboni.   

Msaada huo umehusisha unga wa ngano, unga wa mahindi, mafuta ya kipikia, sukari na maji ya kunywa.                                               

Mwenyekiti huyo amesema ni sehemu ya utaratibu wa taasisi hiyo kutembelea na kutoa msaada kwa yatima ikiwa wanafanya hivyo mara mbili kwa mwaka.

“Kwa mwezi huu wa Desemba tumetembelea vituo sita vyote kutoka Wilaya ya Kigamboni, pamoja na kuwapatia zawadi ili kupeleka furaha kwa watoto hawa,” amesema Ally.

Amesema Wilaya ya Kigamboni ina vituo 10 vya watoto yatima, hata hivyo wameweza kutoa misaada kwa sita pekee.

“Kama watu wapo tayari kusaidia watoto hawa sisi tupo tayari kushirikiana nao na tutamuonesha vituo vyote 10, kwani jukumu la kuwalea watoto hawa la sisi wote,” ameongeza.

Elizabeth Moses, ambaye ni msimamizi wa Kituo cha Jerusalem chenye watoto 32, ameshukuru kwa msaada huo na kusema wamepata msaada wakati muafaka hasa kipindi hiki cha sikukuu.

“Tunashukuru Mungu kwa upendo ambao umeoneshwa na watu walitupatia hii misaada kwani ni kitu kizuri walichofanya na Mungu atawalipa pale walipotoa,” amesema Elizabeth.

Sauda Juma, ambaye ni mlezi wa Kituo cha Amani Foundation, chenye watoto 56 amefurahi kwa kupata zawadi hizo kutoka kwa wadau mbalimbali.

“Tunashukuru kwa bidhaa mlizotupatia sisi tumefurahi sana na hatuna cha kuwalipa bali Mungu ndiyo atawalipa,” amesema Sauda.

Ameendelea kwa kusema kwamba, ameomba kwa taasisi nyingine kujitokeza kwa kutoa misaada kwa watoto yatima kwani wao pia wanahitaji upendo, faraja na amani.

Mmoja wa watoto yatima katika kituo hicho, Zawadi Joseph ametoa shukrani kwa zawadi hizo akiwaomba wananchi kutochoka kuwasaidia.

Mwenyekiti Mtaa wa Maweni, Shabani Mzuwanda amewashukuru Wajomba Family, kwa kujitoa kwao kuwasaidia watoto walio kwenye eneo lake kwani anaamini msaada huo utakwenda kusaidia kwa muda.

“Kusaidia watoto ni jambo nzuri sana kwani kuna faraja tunaipeleka ndani ya watoto hawa, kwa hapa Kigamboni vituo vipo vingi lakini mimi nashukuru kituo cha hapa mtaani kwangu kubahatika kupata msaada huu,” amesema Mzuwanda.

Related Posts