Kauli ya Warioba kifo cha Jaji Werema

Dar es Salaam. Jaji mstaafu, Joseph Warioba amemzungumzia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mstaafu Jaji Frederick Werema akisema ni miongoni mwa watu wachache aliowahi kufanya nao kazi kwa uaminifu, weledi, uadilifu na uwazi mkubwa.

“Pamoja na kwamba amekuwa akitajwa kwenye sakata la Escrow, hakuna mtu anayeweza kutilia shaka uaminifu wake, ni mtu mkweli bahati isiyokuwa nzuri tumempoteza katika umri ambao mawazo yake yalikuwa yanategemewa zaidi. Wengine sisi tumepoteza mtu wa karibu,” amesema.

Jaji Warioba amesema hayo jijini Dar es Salaam leo Desemba 31, 2024 alipokwenda nyumbani kwa Jaji Werema aliyefariki dunia jana Desemba 30, 2024 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.

Amesema Jaji Werema aliingia serikalini kama mtumishi wa umma kati ya mwaka 1984 au 1985 wakati huo yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), lakini hakukaa naye kwa muda mrefu.

Jaji Warioba amesema baada ya majukumu yake kama AG, alikuwa Waziri Mkuu lakini alikuja kuwa karibu na Jaji Werema kwenye Tume ya Rushwa kwa kuwa alikuwa miongoni mwa waandamizi katika chombo hicho.

“Taarifa ya tume waliyoiandaa alikuwa ni Jaji Werema na aliyekuwa Katibu Mkuu Alex kwa wakati huo, walifanya kazi kubwa na ni miongoni mwa taarifa zilizoandaliwa kwa umakini mkubwa katika kutoa mapendekezo.

“Baada ya kazi ya tume ile, na taarifa kusambaa duniani nikiwa Waziri Mkuu mwaka 1998, niliombwa na Global Coalition Africa kuandaa waraka ambao ungekuwa msingi wa mapambano ya rushwa,” amesema.

Global Coalition Africa ni muungano wa kimataifa ulioanzishwa ili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu maendeleo ya Bara la Afrika ukishirikisha kada mbalimbali.

Jaji Warioba amesema wakati taasisi hiyo ilipomuomba alikuwa Jaji (katika Mahakama ya Kimataifa ya Sheria za Bahari iliyoko Hamburg, Ujerumani, kuanzia mwaka 1996 hadi 1999), hivyo alimtwisha jukumu hilo Jaji Werema aandae waraka ampelekee. Amesema aliuangalia na alifanyia marekebisho mambo machache.

“Baada ya kurekebisha niliupeleka Global Coalition bahati isiyokuwa nzuri wakati wananiomba kwenda kufanya wasilisho nilikuwa nje na majukumu mengine ndipo nilimrejea tena Jaji Werema akatekeleze jukumu hilo,” amesema.

Amesema mwaka uliofuatia Global Coalition waliandaa semina kubwa nchini Marekani na kuwaita mawaziri wa nchi za Afrika kwenda kupata mafunzo jinsi ya kukabiliana na rushwa katika mataifa yao.

“Paper (waraka) tuliyoiandaa ilikuwa msingi wa mafundisho hayo, katika mazungumzo ya semina hiyo yalitoka na maazimio ya njia ya kukabiliana na rushwa na ilifikia hatua paper hiyo ilipelekwa kwenye mikutano mikubwa na kutumiwa na viongozi wa Marekani,” amesema.

Jaji Warioba amesema matokeo ya semina hizo ulikuwa msingi dhabiti wa kutengeneza mikataba mbalimbali ikiwemo ya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Wengi hawajui wazo la kwanza lilitokana na Jaji Werema lakini niwaambie ni yeye ndiye aliwasha kiberiti, ambaye alikuwa anafanya kazi kwa uadilifu, maadili, nidhamu na alikuwa muwazi,” amesema.

Amesema Jaji Werema alikuwa hawezi kusema kitu hiki cheupe wakati cheusi na ilikuwa akikupatia ushauri anautoa kwa jinsi anavyoona inafaa.

“Jaji Werema nilikuwa naye karibu tangu miaka ya 1990, tulikuwa na ushirikiano mzuri na hata juzi hapa nilipata matatizo ya kuunguliwa na nyumba yangu alikuja kuniona na tulikaa kuzungumza kama saa mbili hivi,” amesema.

Amesema baada ya mazungumzo walijadiliana umuhimu wa kwenda kuchunguza afya zao.

Related Posts