Mahakama Korea Kusini yatoa hati Rais Yoon akamatwe

Seoul. Mahakama mjini Seoul nchini Korea Kusini imetoa hati ya kukamatwa kwa aliyekuwa Rais wa taifa hilo, Yoon Suk Yeol ambaye aling’oka madarakani Desemba 3, 2024.

Rais Yoon aling’oka madarakani siku chache baada ya kutangaza amri ya taifa hilo kuongozwa chini ya utawala wa Sheria ya Kijeshi (Martial Law) uamuzi ambao ulipingwa vikali na wananchi na wanasiasa wa upinzani nchini humo.

Hati ya kukamatwa kwa Rais Yoon ilitolewa jana ambapo inaainisha moja ya mashtaka yanayomkabili juwa ni pamoja na shtaka la uasi na uhaini na kupuuza wito wa mahakama mara tatu katika pindi cha wiki mbili zilizopita.

Hatua hiyo ya mahakama ni kujibu ombi la mamlaka zinazoendesha uchunguzi dhidi ya mwanasiasa huyo lililoiomba mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwa Yoon kwa mashtaka ya uasi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Ombi hilo la wachunguzi wanaofuatilia mashtaka anayokabiliwa nayo Yoon limeelezwa na wakili wa Rais huyo kuwa ni jambo linalifanyika “kinyume cha sheria.”

Korea Kusini ambayo juzi ilipata pigo kufuatia ajali ya ndege ya Shirika la Jeju kupata ajali na kusababisha vifo vya watu 179 na wengine wawili wakinusurika, imekuwa katika mtikisiko wa kisiasa huku Yoon na Rais wa mpito, Han Duck-soo, wote waking’olewa madarakani.

Yoon ni Rais wa kwanza wa Korea Kusini aliyekuwa madarakani kukabiliwa na hati ya kukamatwa.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, Wachunguzi wana muda hadi Januari 6, 2025, wa kutekeleza hati hiyo na wanaweza kuomba muda wa ziada.

Hata hivyo, haijulikani kama watafanikiwa kutekeleza hati hiyo, kwani wanaweza kuzuiwa na timu ya usalama ya rais huyo na wafuasi wanaomkingia kifua.

Huduma ya usalama ya rais hapo awali iliwazuia wachunguzi kuingia katika ofisi ya rais na makazi binafsi ya Yoon kufanya upekuzi uliodhibitishwa na mahakama.

Hapo awali, mamlaka za Korea Kusini ziliwahi kusitisha jitihada za kukamata wanasiasa maarufu baada ya wasaidizi wao na wafuasi kuzuia polisi kwa nguvu.

Jumatatu, timu ya kisheria ya Yoon ilisema wachunguzi hawana mamlaka ya kumkamata, kwani kutangaza hali ya hatari ya kijeshi ni mojawapo ya mamlaka ya rais kwa mujibu wa katiba.

Yoon alitetea uamuzi wake wa kutangaza hali ya hatari ya kijeshi na akaapa kupambana hadi mwisho, ingawa alisema pia hatakwepa majukumu yake ya kisheria na kisiasa.

“Wabunge wote pigeni kura ya kumuondoa Rais Yoon, lazima asimamishwe madarakani mara moja” alisema Han Dong-hoon Desemba 13.

Wakili wake, Yun Gap-geun, amesema kutofika kwa Yoon kwa wito wa mahojiano matatu ya awali kulisababishwa na wasiwasi wa halali.

Mahali alipo Yoon kwa sasa hapajulikani hadharani, lakini amezuiwa kuondoka nchini.

Ingawa amesimamishwa kutekeleza majukumu ya urais tangu Desemba 14 mwaka huu baada ya wabunge kupiga kura ya kumwondoa, anaweza tu kuondolewa rasmi iwapo mahakama ya katiba itaidhinisha uamuzi huo.

Kwa sasa, kuna majaji sita tu kati ya tisa wanaohitajika katika mahakama ya katiba. Hii ina maana kwamba kura moja ya kupinga inaweza kumwokoa Yoon asiondolewe madarakani.

Wabunge wa upinzani walitarajia uteuzi wa majaji watatu wa ziada ungeongeza nafasi za Yoon kuondolewa, lakini pendekezo lao lilipingwa na Waziri Mkuu Han Duck-soo wiki iliyopita.

Tangu wakati huo, upinzani umeamua kupiga kura ya kumwondoa Han, ambaye alikuwa ameanza kuhudumu kama kiongozi wa mpito baada ya Yoon kusimamishwa.

Sasa, wanatishia kufanya hivyo kwa waziri wa fedha Choi Sang-mok, ambaye kwa sasa ni kaimu rais na waziri mkuu wa mpito.

Related Posts