Tanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linamsaka Mwita Yoba kwa tuhuma za kuteketeza nyumba kwa moto na kusababisha vifo vya watu wanne, wakiwamo mama na watoto wake watatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Desemba 31, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema tukio hilo lilitokea Desemba 30, 2024, saa 4:45 asubuhi, katika Kitongoji cha Kwedichocho kilichopo Kijiji cha Manga, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Kamanda Mchunguzi ameeleza kuwa, walifariki dunia katika tukio hilo ni mama wa watoto hao, Pili Saguge (28), mkulima na mkazi wa Kwedichocho, pamoja na watoto Chacha Nyabilenga, Jane Nyabilenga na Makabala Nyabilenga.
Kamanda Mchunguzi amefafanua kuwa, chanzo cha tukio hilo ni mtuhumiwa huyo kudai kuwa familia hiyo ilimuua mtoto wake kwa sumu, hali iliyomsukuma kuteketeza nyumba hiyo kwa lengo la kulipiza kisasi.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu mahali alipo mtuhumiwa huyo, kuwasiliana na kituo chochote cha polisi kilicho karibu ili hatua kali za kisheria zichukuliwe mara moja dhidi yake.
Endelea kufuatilia zaidi taarifa kuhusu hili kwenye tovuti na mitandao ya Mwananchi.