Mapinduzi yalivyomkimbiza Sultan Jamshid | Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati Wazanzibari wakikaribia kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi, historia inamkumbuka sultani wa mwisho wa visiwa hivyo, Sayyid Jamshid bin Abdullah Al Said aliyefariki dunia jana nchini Oman akiwa na umri wa miaka 95.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya kimataifa zimesema kuwa Sultan Jamshid alifariki jioni ya Desemba 30, 2024 katika Hospitali ya Kifalme huko Muscat, Oman.

Mwili wake umezikwa leo Desemba 31 katika makaburi ya Kifalme yaliyopo Muscat.

Kifo cha Sultan Jamshid kinahitimisha sura ya kihistoria ya maisha ya Sayyid Jamshid, ambaye alihamia uhamishoni nchini Uingereza baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyokomesha utawala wa kisultani visiwani Zanzibar.

Sultani Jamshid bin Abdullah Al Said aliyezaliwa Septemba 16, 1929 alikuwa Sultani wa 10 na wa mwisho wa Zanzibar, sehemu ya ukoo wa Al Said, ambao ulitawala Zanzibar na Oman.

Alipata elimu yake ya msingi Zanzibar na baadaye aliendelea na masomo nchini Misri na Uingereza ambako baada ya msomo alihudumu katika jeshi la wanamaji kwa takriban miaka miwili.

Alirejea Zanzibar katika miaka ya mwisho ya utawala wa babu yake Sultani Sayyid Khalifa aliyetawala kutoka Oktoba 1960 mpaka Julai 1963 alipofariki na kiti chake kurithiwa na Jamshid.

Jamshid alipata madaraka ya usultani Julai 1, 1963, baada ya Zanzibar kupata uhuru kutoka kwa utawala wa Uingereza, akiongoza kifalme visiwa hivyo.

Hata hivyo, utawala wake haukudumu kwani ulikumbwa na changamoto za kisiasa na kijamii kutokana na historia changamani ya Zanzibar na mgawanyiko wa watu –Waarabu, Waafrika, Wahindi na Wazungu.

Serikali yake ilikumbana na matatizo ya migawanyiko ya muda mrefu kati ya wasomi wa asili ya Kiarabu, ambao kwa jadi walikuwa na mamlaka, na walio wengi wa Kiafrika, ambao walitaka ushirikishwaji mkubwa wa kisiasa na kiuchumi.

Januari 12, 1964, miezi sita tu baada ya kuwa Sultani, aling’olewa kwenye mapinduzi yaliyofanywa na vikosi vya kitaifa vya Kiafrika na hivyo kumaliza utawala wa Waarabu zaidi ya miaka 200.

Mapinduzi hayo yaliwezesha kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Pemba, ambayo baadaye iliungana na Tanganyika na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mapinduzi yalivyomkimbiza

Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyotokea Januari 12, 1964, ilikuwa tukio la kihistoria ambalo liliangusha utawala wa kifalme wa Kiarabu uliokuwa chini ya Sultani Jamshid.

Mapinduzi hayo yaliongozwa na John Okello, aliyewaongoza vijana wanamapinduzi wakiwemo vijana waliokuwa wakipinga utawala wa kifalme wa Kiarabu na ukandamizaji wa watu wenye asili ya Kiafrika.

Hali hiyo ilisababishwa na mvutano wa siasa na kijamii uliochochewa na uchaguzi wa Julai 1963, ambapo vyama vinavyowakilisha Waarabu na Wahindi vilipata mamlaka licha ya kuwa wenye asili ya Kiafrika walikuwa wengi.

Katika uchaguzi huo, vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilichopata viti 12 na Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP) kilichopata viti sita viliunganisha viti hivyo na kupata 18 na hivyo kuishinda Afro Shiraz Party (ASP) iliyokuwa na viti 13.

Baada ya kuunganisha viti hivyo, chama cha ZNP kilitoa Waziri Mkuu wa kwanza wa visiwa hivyo, Mohammed Shamte aliyekuwa chini ya Serikali ya Sultan Jamshid.

Hata hivyo, ASP ilikuwa imepata jumla ya asilimia za kura 54.21, ZNP asilimia 29.85 na ZPPP asilimia 15.94.

Matokeo hayo yalichangia kwa kiasi kikubwa kuibuka kwa machafuko ya kisiasa yaliyochochea Mapinduzi ya Zanzibar.

Siku ya mapinduzi, wapiganaji walivamia ofisi za Serikali, kasri ya kifalme na vituo vya polisi.

Sultani Jamshid bin Abdullah Al Said, aliyekuwa na umri wa miaka 34 wakati huo, kwa msaada wa maofisa wa Uingereza, alisafirishwa kwenda uwanja wa ndege na kuondoka Zanzibar kwa ndege.

Baada ya hapo, alihamia Oman, lakini hakupata hifadhi ya kudumu huko, kwani wakati huo pia kulikuwa na mzozo wa kisiasa.

Hatimaye, alikimbilia Uingereza, ambako alikaa uhamishoni pamoja na familia yake kwa miongo mingi.

Kwa mujibu wa BBC, Jamshid aliishi uhamishoni nchini Uingereza katika jiji la Portsmouth kwa miaka 56.

Gazeti la The Guardian la Uingereza linaeleza kuwa Jamshid alikataliwa mara kadhaa maombi yake ya kutaka kuishi Oman japo watu wa familia yake waliruhusiwa kuishi nchini huko tangu miaka ya 1980.

Hata hivyo, mwaka 2020 na Serikali ya Oman ilimruhusu kurejea katika nchi hiyo ya asili ya familia yake.

Kwa kipindi chote alichoishi Uingereza inaripotiwa kuwa Jamshid aliishi kwa ukimya na hata baadhi ya jirani zake hawakujua yeye ni nani.

Rais wa zamani wa Zanzibar (1990w-2000) Dk Salmin Amour alimruhusu Jamshid kurejea Zanzibar kama raia wa kawaida lakini hakufanya hivyo.

Sultan Jamshid bin Abdullah Al Said wa Zanzibar alikuwa wa ukoo wa Al Said, ambao ulitawala Oman na Zanzibar karne nyingi na mwaka 1840 Sultan Seyyid Said alihamishia makao makuu yake Zanzibar.

Babu yake aliyeitwa Sultani Hamoud bin Mohammed Al Said alikuwa Sultani wa Zanzibar kuanzia 1896 hadi 1902.

Anajulikana sana kwa kufuta biashara ya utumwa Zanzibar chini ya ushawishi wa Waingereza na kuleta mabadiliko ya utawala wa kisasa huku akiendeleza uhusiano na Dola ya Uingereza.

Bibi Sayyida Khanfora bint Majid Al Said alikuwa binti wa Sultani Majid bin Said, Sultani wa kwanza wa Zanzibar (alitawala 1856–1870) baada ya kifo cha baba yake Sultan Sayyid Said.

Wazazi hawa wa mababu walimweka Jamshid katika nasaba iliyoonyesha uongozi wa Oman na urithi wa kipekee wa kitamaduni wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa BBC, baada ya kufariki kwa Sayyid Said mwaka 1856, kukatokea ugomvi wa madaraka baina ya wototo wake wawili, Majid na Thuwain. Chini ya makubaliano yaliyosimamiwa na Waingereza, wakaigawa dola ya baba yao katikia nchi mbili ambapo, Majid akawa Sultani wa Zanzibar na Thuwain akawa Sultani wa Oman.

Japo utawala wa familia hiyo ulikomeshwa Zanzibar Januari 12, 1964 kwa kupinduliwa, nchini Oman bado familia hiyo inaendelea kutawala.

Related Posts